Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabingwa Ulaya... Ukizubaa unaachwa

UEFA Pict

Muktasari:

  • Wakati Arsenal tayari ikiwa imefuzu salama kwenda hatua ya 16 bora, ambako wataungana na Bayern Munich, timu nyingine zote bado zina kazi ya kufanya katika msimamo uliosongamana wa ligi yenye timu 36.

LONDON, ENGLAND: HALI ni tete katika kuelekea siku ya mwisho inayotarajiwa kuwa ya kusisimua sana katika hatua ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku timu 30 bado zikisubiri kuamua hatima zao. Shughuli hiyo pevu itapigwa Jumatano.

Wakati Arsenal tayari ikiwa imefuzu salama kwenda hatua ya 16 bora, ambako wataungana na Bayern Munich, timu nyingine zote bado zina kazi ya kufanya katika msimamo uliosongamana wa ligi yenye timu 36.

Liverpool, Tottenham, Newcastle United na Chelsea ni klabu nyingine za Ligi Kuu England zilizo ndani ya nane bora kwa sasa, nafasi ambayo ingewafanya waepuke hatua ya mtoano (play-offs) na kwenda moja kwa moja hatua ya 16 bora.

Manchester City, waliopo kwa sasa kwenye nafasi ya mtoano wako nyuma ya Newcastle na Chelsea kwa tofauti ya mabao tu, kama sehemu ya kundi la timu nane zilizo na pointi 13 kuelekea raundi ya mwisho Jumatano. Haijawahi kutokea klabu sita kutoka nchi moja kushiriki mashindano haya kwa wakati mmoja, achilia mbali kufika hatua ya mtoano.

UE 01

Nani tayari amefuzu kwenda hatua ya 16 bora? Vinara Arsenal wameshinda mechi zao zote saba na pointi moja tu nyumbani dhidi ya Kairat Almaty itawatosha kuhakikisha nafasi ya juu mbele ya Bayern. Kwa upande wa upangaji wa hatua ya 16 bora, nafasi ya kwanza au ya pili haina tofauti kubwa, kwani timu mbili za juu zitapangwa pamoja kwenye droo na kukutana na washindi wa mechi za mtoano kati ya timu za nafasi ya 15 na 18 au 16 na 17 mtawalia.

Bayern wanahitaji pointi moja ugenini dhidi ya PSV Eindhoven ili kuhakikisha wanamaliza katika nafasi mbili za juu.

Timu mbili za juu zina uhakika wa kucheza mechi ya marudiano nyumbani katika kila raundi hadi fainali.

Benfica ya Jose Mourinho kwa sasa wako nje ya nafasi za mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na inashika nafasi ya tatu katika ligi ya Ureno, wakiwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya vinara Porto.

Mapambano ya kuingia nane bora. Hapa ndipo mambo yanapovutia zaidi. Kwa kuanzia na sehemu iliyo wazi zaidi: Real Madrid na Liverpool (zote zikiwa na pointi 15), pamoja na Tottenham (pointi 14), ushindi katika mechi ya nane utawapa tiketi ya moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora.

Tottenham itacheza ugenini dhidi ya Eintracht Frankfurt ambao tayari wameondolewa, katika uwanja ambao Spurs walishinda mwaka jana njiani kuelekea ubingwa wa Europa League uliowapa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

UE 02

Liverpool ya Arne Slot itakuwa nyumbani dhidi ya Qarabag, ambao bado wana nafasi ya kuingia nane bora. Real Madrid itakuwa ugenini dhidi ya kocha wao wa zamani Jose Mourinho na Benfica yake. Mourinho alifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo akiwa Real Madrid kabla ya kuondoka mwaka 2013, lakini Benfica iliyoshinda mara mbili tu katika mechi saba za kwanza, inahitaji kuifunga Real Madrid ili kuwa na nafasi ya kuingia mtoano.

Nyuma ya Spurs kuna kundi la timu nane, kuanzia mabingwa watetezi Paris Saint-Germain walio nafasi ya sita hadi Atalanta walio nafasi ya 13, zote zikiwa na pointi 13. Newcastle, Chelsea na Manchester City zote zimo kwenye kundi hilo na zinahitaji ushindi na hata hivyo, hatima yao inaweza kuamuliwa kwa tofauti ya mabao. Chelsea pia watakutana na kocha wao wa zamani Antonio Conte, aliyeshinda Serie A na Napoli msimu uliopita, lakini sasa atawakaribisha The Blues mjini Naples huku timu yake ikiwa nje ya nafasi za mtoano kwa tofauti ya mabao.

Man City watawakaribisha Galatasaray, wakati Newcastle ya Eddie Howe wanakabiliwa na safari ngumu ya ugenini dhidi ya PSG. Kila timu hadi Qarabag walioko nafasi ya 18 bado ina nafasi ya kihesabu ya kufuzu moja kwa moja. Hii ni kwa sababu, cha kushangaza, licha ya timu 16 kuwania nafasi sita zilizobaki za nane bora, ni mechi mbili tu kati ya 18 zitakazochezwa Jumatano zitakuwa kati ya timu zinazokabiliana moja kwa moja. Safari ya Newcastle kwenda Paris ni moja, na Borussia Dortmund wakiwa nyumbani dhidi ya Inter Milan ni nyingine.

UE 03

Mapambano ya kuingia mtoano (Play-offs). Pambano la kuingia mtoano pia ni kali sana, huku kila timu hadi Ajax walioko nafasi ya 32 bado ikiwa kwenye mbio. Ni timu nne tu za mwisho, Eintracht Frankfurt, Slavia Prague, Villarreal na Kairat ndizo tayari zimeondolewa.

Ni pointi tatu tu zinazotenganisha Marseille walioko nafasi ya 19 na Ajax, huku hata Dortmund walioko nafasi ya 16 wakiwa mbele kwa pointi mbili dhidi ya Marseille na bado wakiwa na matumaini madogo ya kuingia nane bora hawajathibitisha rasmi nafasi ya mtoano. Tena, ratiba imeangukia kwa namna ambayo ni mechi mbili tu zitakuwa mapambano ya moja kwa moja kati ya wanaowania mtoano Ajax dhidi ya Olympiakos na Marseille ugenini dhidi ya Club Brugge.

MECHI ZA RAUNDI YA

MWISHO JUMATANO

Ajax v Olympiakos

Arsenal v Kairat

Athletic Club v Sporting

Atletico Madrid v Bodo/Glimt

Barcelona v Copenhagen

Bayer Leverkusen v Villarreal

Benfica v Real Madrid

Borussia Dortmund v Inter Milan

Club Brugge v Marseille

Eintracht Frankfurt v Tottenham

Liverpool v Qarabag

Manchester City v Galatasaray

Monaco v Juventus

Napoli v Chelsea

PSV Eindhoven v Bayern Munich

Pafos v Slavia Prague

Paris St-Germain v Newcastle

Union Saint-Gilloise v Atalanta

Mechi zote zitaanza saa 5:00 usiku