Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maandalizi AFCON 2027, Kenya kuwasilisha Sh78 bilioni CAF

KENYA Pict

Muktasari:

  • Ada hiyo ni sehemu ya makubaliano ya zabuni ya pamoja ya East Africa Pamoja, iliyoipa Kenya haki ya kuandaa mashindano hayo kwa ushirikiano na Uganda na Tanzania. Wakati mataifa hayo jirani tayari yameshawasilisha mchango wao wa dola milioni 30 (Sh78 bilioni) kila moja, Kenya bado iko katika hatua za mwisho kukamilisha wajibu huo.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), linatarajia kupokea dola milioni 30 (Sh78 bilioni) kutoka Kenya kama sehemu ya wajibu wa kifedha unaotokana na makubaliano ya kuandaa kwa pamoja Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Ada hiyo ni sehemu ya makubaliano ya zabuni ya pamoja ya East Africa Pamoja, iliyoipa Kenya haki ya kuandaa mashindano hayo kwa ushirikiano na Uganda na Tanzania. Wakati mataifa hayo jirani tayari yameshawasilisha mchango wao wa dola milioni 30 (Sh78 bilioni) kila moja, Kenya bado iko katika hatua za mwisho kukamilisha wajibu huo.

Kwa mujibu wa mkataba wa uenyeji, kila nchi inapaswa kuwasilisha mchango wake kabla ya Aprili 2026. Kamati ya Maandalizi ya Ndani (LOC) ya Kenya imeeleza kuwa malipo hayo ni muhimu ili kulinda hadhi ya nchi kama mwenyeji na kuepusha wasiwasi wowote kutoka CAF. 

Fedha hizo zinahitajika kufanikisha maandalizi makubwa ya mashindano, yakiwemo ujenzi na ukarabati wa viwanja, kuboresha viwanja vya mazoezi, uratibu wa usalama na maboresho ya miundombinu ya usafiri katika miji itakayokuwa mwenyeji.

Mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027 yatakayokuwa na timu 28, yanahitaji maandalizi ya hali ya juu katika nyanja za kiutendaji na miundombinu, huku CAF ikiendelea kufuatilia kwa karibu utayari wa nchi zote tatu washirika.

Timu za ukaguzi kutoka CAF zimekuwa zikitembelea kumbi mbalimbali za michezo katika ukanda huo kukagua viwango vya viwanja, maeneo ya mazoezi, mifumo ya usalama na miundombinu inayosaidia mashindano.

Nchini Kenya, viwanja vilivyokaguliwa ni pamoja na Kasarani, Nyayo, Talanta Sports na Ulinzi Sports Complex ambavyo vimetengwa kwa shughuli za mashindano hayo.

Hata hivyo, hitaji hilo la kifedha limeibuka wakati mgumu kwa sekta ya michezo nchini Kenya.

Makadirio ya bajeti ya mwaka 2025-2026 yanaonesha kuwa Idara ya Serikali ya Michezo imepunguziwa mgao kwa Sh1.1 bilioni, kutoka Sh18.59 bilioni hadi Sh17.46 bilioni za Kenya.

Marekebisho hayo hayakujumuisha Sh3.9 bilioni 3.9 zilizotengwa kwa ada ya haki za uenyeji wa AFCON, hali inayoiweka wizara bila rasilimali za kutosha kufikia Aprili 2026.

Wizara ya Michezo Kenya imekiri kuwa ingawa mikataba ya uenyeji wa AFCON 2027 iko tayari kusainiwa, mchakato umekwama kutokana na kukosekana kwa kifungu maalum cha bajeti kwa ajili ya ada hiyo. Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Bunge imeeleza kuwa ufinyu wa bajeti ya taifa unazuia kuongeza mgao kwa wizara mbalimbali.

Maafisa wa LOC wanasema kuwa bajeti ya serikali kwa ujumla inapunguza uwezekano wa kupata fedha za nyongeza, hivyo kuifanya serikali kulazimika kufikiria upya mgawanyo wa rasilimali kutoka sekta nyingine.

Historia ya Kenya katika kuandaa mashindano ya bara inaongeza uzito wa hali ilivyo. Mwaka 2018, CAF iliinyang’anya Kenya haki ya kuandaa Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) baada ya kubainisha kuchelewa kwa ukarabati wa viwanja, kutofikiwa kwa viwango vya miundombinu na kushindwa kutimiza dhamana za kiserikali. Hatimaye, mashindano hayo yaliandaliwa na Morocco.

Iwapo Kenya itashindwa kuwasilisha ada ya Shilingi bilioni 3.9 (dola milioni 30) ndani ya muda uliowekwa kimkataba, CAF itakuwa na mamlaka ya kutoa notisi ya ukiukwaji wa makubaliano. Kwa kuwa AFCON 2027 ni mradi wa pamoja, shirikisho hilo linaweza kuamua kurekebisha mpangilio wa uenyeji badala ya kufuta kabisa mashindano hayo kwa nchi zote tatu.

Hatua kama hiyo inaweza kupunguza nafasi ya Kenya katika uenyeji, huku baadhi ya mechi zikahamishiwa Uganda na Tanzania. Mbali na athari za kimichezo, hatua hiyo pia inaweza kudhoofisha fursa za kibiashara za Kenya na kuathiri hadhi yake katika zabuni za baadaye za kuandaa mashindano ya bara au kimataifa.