Masharti ya Chelle kupelekwa Kamati ya Ufundi NFF
Muktasari:
- Chelle bado ana mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake wa sasa, lakini mjadala kuhusu mustakabali wake wa muda mrefu umechochewa na mafanikio ya Nigeria katika michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika Morocco, ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya tatu.
MJUMBE wa Bodi ya Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) amethibitisha kuwa, masharti yaliyowasilishwa na kocha mkuu wa timu ya taifa hilo, Eric Chelle, yatafanyiwa tathmini na Kamati ya Ufundi ya NFF kabla ya uamuzi wowote kufikiwa.
Chelle bado ana mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake wa sasa, lakini mjadala kuhusu mustakabali wake wa muda mrefu umechochewa na mafanikio ya Nigeria katika michuano ya AFCON 2025 iliyofanyika Morocco, ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya tatu.
Super Eagles ilionyesha kiwango cha juu kwa kucheza mechi saba bila kupoteza, kabla ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya wenyeji, timu ya taifa ya Morocco, katika nusu fainali. Aidha, iliweka rekodi ya kufunga mabao 14, idadi kubwa zaidi kuwahi kufungwa na Nigeria katika kampeni moja ya AFCON.
Licha ya kuungwa mkono hadharani na baadhi ya viongozi wa NFF, taarifa zinaeleza kuwa Chelle anawaniwa pia na mataifa mengine barani Afrika, huku baadhi ya vyama vya soka vikidaiwa kuwa tayari kutoa mshahara wa takribani dola 100,000 (Sh258 milioni) kwa mwezi. Pia amehusishwa kwa mbali na uwezekano wa nafasi nchini Ufaransa baada ya kubadili wakala wake.
Kwa mujibu wa ripoti, Januari 22, 2026 Chelle aliwasilisha orodha ya masharti 19 kama sehemu ya majadiliano ya kuongeza mkataba wake.
Miongoni mwa masharti hayo ni kupatiwa gari binafsi (SUV) lenye dereva na ulinzi, makazi katika eneo salama lenye umeme wa uhakika, ofisi kamili yenye projector kwa mikutano ya kiufundi, tiketi za ndege kwa familia yake, pamoja na uhuru kamili wa kuchagua kikosi na mechi za kirafiki.
Pia anataka ruhusa ya kufuatilia ligi ya ndani ili kusaka vipaji kwa timu ya wakubwa na makundi ya vijana (U-23, U-20 na U-17), huku msaidizi wake binafsi akijumuishwa katika mfumo wa bonasi na posho.
Akizungumza na gazeti la The PUNCH, mjumbe huyo wa Bodi ya NFF amesema: “Tusisahau kuwa Chelle bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake. Haya ni masharti mapya yanayohitaji kuzingatiwa kwa ajili ya kuongeza mkataba, na ni suala la kamati ya ufundi kuyapitia kabla ya kuwasilishwa kwa bodi kwa uamuzi wa mwisho.”
Nje ya mazungumzo hayo, Chelle ameacha kufanya kazi na wakala wake wa awali, Abraham Sidibe, na sasa anawakilishwa na Kampuni ya Wilders Sport yenye makao yake Marseille nchini Ufaransa.
Kocha huyo anatarajiwa kutangaza kikosi kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Jordan itakayochezwa mwezi ujao, kati ya Machi 23 na 31, 2026.
Wakati huohuo, Super Eagles inasubiri uamuzi wa FIFA kuhusu malalamiko yao dhidi ya timu ya taifa ya DR Congo, ikidaiwa kuwa ilitumia wachezaji wasiostahili katika mechi ya mchujo wa Afrika kuelekea Kombe la Dunia 2026.
Uamuzi chanya unaweza kuifanya Nigeria kusonga mbele hadi hatua ya mchujo wa kimataifa nchini Mexico, jambo litakalobadilisha kwa kiasi kikubwa ratiba yao ya kimataifa.