Maajabu ya Bruno Manchester United ni balaa kubwa

MANCHESTER, ENGLAND. MWAKA mmoja umepita, Manchester United tangu walipoanza mchakato wa kurudi anga za juu katika soka, lakini ni baada ya mwokozi wao kutua.
Huyo ni Bruno Fernandes, aliyewasili Old Trafford akitokea Sporting Lisbon kwa ada ya Pauni 55 milioni na tangu wakati huo ni mwaka sasa.
Bruno Fernandes nd’o chanzo cha tabasamu la mashabiki wa Man United kwa sasa, wakiwa kwenye mchuano wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.
Kabla Fernandes hajatua, wiki moja nyuma Man United ilitoka kula kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Burnley na wakati huo, Solskjaer alikuwa kwenye hali mbaya na mashabiki walianza kupiga kelele afukuzwe.
Matokeo hayo yaliwafanya washike nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, pointi 24 nyuma ya vinara wa wakati huo, Liverpool na matumaini yalikuwa hafifu sana kwamba mambo yatabadilika.
Lakini, baada ya kutua tu Fernandes, mambo yalibadilika.
Baada ya ujio wa Fernandes, Man United ilimaliza msimu kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi na kufika nusu fainali tatu.
Msimu huu, Fernandez ameendeleza makali yake na Man United kwa wakati huu ni moja ya timu zinazotajwa kwenye mbio za ubingwa wa ligi.

Tangu Fernandes atue Man United, hakuna mchezaji yeyote kwenye Ligi Kuu England aliyefunga mabao mengi kumzidi, akiwa amefunga mara 28 katika michuano yote. Hata straika mtupiaji, Harry Kane amefunga mara 26 tu ndani ya muda huo, huku Kevin De Bruyne pekee ndiye aliyemzidi Fernandes kwa asisti, 21 kwa 17.
Ndani ya muda huo, ukiacha mechi ya jana dhidi ya Arsenal, Fernandes ameichezea Man United mechi 34 kwenye Ligi Kuu England na chama lake limeshinda 21 kati ya hizo. Kabla ya ujio wake, mechi kama hizo 34, Man United ilikuwa imeshinda 12 tu.
Kwa kutazama mwaka mmoja wa Fernandes kwenye kikosi cha Man United na mchango wake, kocha Solskjaer amebaki kumwaga sifa tu.
Alisema: “Safi sana. Tangu siku ya kwanza aliyokuja ameamsha hamasa kubwa. Ni ingizo muhimu sana. Ni mtu mtulivu, anapiga sana kazi na nadhani kila mtu analiona hilo ndani ya uwanja.
Nimevutiwa na mwaka wake huu wa kwanza na nina imani ataendelea hivi kwa muda mrefu zaidi.”
Fernandes amebadili mengi kuhusu Man United kuanzia ndani ya uwanja hadi nje ambako kulikuwa na mashabiki ambao walikuwa wakiikosoa na kuisakama. Sasa kila kitu kimebadilika na mwepesi wa kukosoa wenzake wanapofanya makosa ya kijinga, mfano Victor Lindelof aliporuhusu Man United kufungwa bao la pili la kizembe kwenye nusu fainali ya Europa League dhidi ya Sevilla. Fernandes hakupenda na kuonyesha hasira zake hapohapo dhidi ya Lindelof. Anataka matokeo mazuri katika kila mechi na wachezaji wenzake wameanza kumwolewa vile Man United inavyopaswa kuwa.
Solskjaer alisema: “Anatazama kila mechi kwenye TV, hasa mechi kubwa. Ukimuuliza ulitazama mechi ya jana usiku? Yeye siku zote anaangalia mechi. Ataendelea kuwa hivi kwa maisha yake yote ya soka, nina uhakika.”