Ferdinand, Crouch wawekeana mzigo England

LONDON, ENGLAND. We unakaa upande gani? Upande wa Rio Ferdinand au Peter Crouch? Wawili hao, Ferdinand amebeti na Crouch kwamba Man United itamaliza juu ya Liverpool kwenye msimu wa Ligi Kuu England msimu huu.
Mshindi atapewa kreti la mvinyo, huku Ferdinand akitamba kwa kusema “Nina uhakika na vijana wangu.”
“Nina uhakika sana na vijana wangu, watakuwa vizuri tu! Watamaliza ligi juu ya Liverpool.”
Wawili hao walikutana wiki hii kwenye studio za BT Sport wakifanya uchambuzi na mtangazaji Jake Humphrey alifichua kidau walilowekeana mastaa hao wa zamani wa Ligi Kuu England.
Kitu kisichoshangaza ni kwamba, mastaa hao wa zamani kila mmoja alivutia upande wa timu yake aliyowahi kuichezea, kwamba itamaliza juu ya mwingine, lakini kubeti kwao huko hakukuhusisha ubingwa.
Crouch alisema: “Subiri, tumesema haihusiani na ubingwa. Nimesema Liverpool itamaliza juu ya Manchester United kwenye msimamo. Sijasema kuhusu ubingwa, lakini nabeti kwamba watamaliza ligi juu ya Manchester United.”
Mchambuzi mwenzao na staa wa zamani wa Ligi Kuu England, Jermaine Jenas aliuliza kama wawili hao walishikana mikono baada ya mechi ya Man United kukumbana na kipigo cha kushtusha nyumbani Old Trafford mbele ya Sheffield United.
Ferdinand alijibu: “Unasema baada ya mechi, mimi nina uhakika. Najiamini na vijana wangu, watakuwa poa. Wanaliza juu ya Liverpool.”
Ushindi wa Liverpool wa mabao 3-1 dhidi ya Tottenham usiku wa juzi Alhamisi uliifanya miamba hiyo ya Anfield, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England kupanda hadi kwenye nafasi ya nne wakiwa na pointi 37 walizovuna kwenye mechi 20. Wapo nyuma kwa nafasi mbili na pointi tatu nyuma ya Man United ya Ole Gunnar Solskjaer, huku katikati ya timu hiyo wamejipenyeza Leicester City wanaoshika nafasi ya tatu.
Manchester City wanashika usukani baada ya kukusanya pointi 41 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Lakini, Jenas, aliyewahi kuichezea Spurs, ameamua kuwavuruga wote, akisema: “Nadhani Spurs itamaliza juu ya timu zote hizo mbili, huo ndo ukweli!”
Baadhi ya mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wametia wasiwasi na maneno ya Ferdinand kwa sababu huko nyuma aliwahi kusema na mambo hayakwenda vizuri.
Shabiki mmoj aliandika: “Rio ni mashine ya mikosi, asante kwa kutuhakikishia kwamba Man United sasa itamaliza nafasi ya nane kwenye msimamo.”
Mwingine alisema: “Rio anapaswa kunyamazishwa - kwanini anajaribu kufanya haya mambo?”
Shabiki wa tatu aliongeza: “Amefanya tena,” huku akiweka emoji za kilio.
Man United leo Jumamosi itakuwa ugenini Emirates kukipiga na Arsenal katika mechi matata kabisa ya Ligi Kuu England, huku kikosi cha Mikel Arteta kikiwa na rekodi nzuri kabisa ya kushinda mechi tano kati ya sita za mwisho. Liverpool wao watacheza kesho Jumapili dhidi ya West Ham United.