Luca Zidane: Babu kafurahi kuja Algeria
Muktasari:
- Zinedine Zidane anafahamika kama mmoja wa wanasoka mahiri kabisa wa Ufaransa, alisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 1998 na alifunga mara mbili kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Brazil katika fainali iliyofanyika Paris.
MARRAKECH, MOROCCO: KIPA, Luca Zidane, mtoto wa gwiji wa soka wa Ufaransa, Zinedine, amesema amepata sapoti kubwa kutoka kwa babu yake juu ya ishu ya kubadili ushiriki wake kwenye soka la kimataifa kuitumikia Algeria baada ya kuichezea Ufaransa kwenye timu za vijana.
Zinedine Zidane anafahamika kama mmoja wa wanasoka mahiri kabisa wa Ufaransa, alisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 1998 na alifunga mara mbili kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Brazil katika fainali iliyofanyika Paris.
Kiungo huyo pia aliiwezesha Ufaransa kushinda ubingwa wa Euro 2000, akipata mafanikio makubwa kabisa akiwa na Les Bleus.
Uamuzi wa kubadili uraia wa Luca, ambaye alikwepa kulinganishwa na baba yake tangu akiwa mdogo kwa kuamua kucheza nafasi ya kipa, umewashangaza wengi baada ya kuchagua kuitumikia Algeria akiwa na umri wa miaka 27.
Na haraka akawa chaguo la kwanza la kipa wa Algeria na baba yake alikuwapo uwanjani kumtazama katika mechi dhidi ya Sudan, ambapo alikiwezesha kikosi cha kocha Vladimir Petković kushinda mechi yake ya kwanza kwenye hatua ya makundi katika Kundi E, ambapo timu hiyo ilishinda 3-0.
Luca Zidane hakupata changamoto nyingi kwenye mechi hiyo, lakini alifanya sevu muhimu dhidi ya Yaser Awad, wakati huo matokeo yalikuwa Algeria ikiongoza 1-0.
"Ninapoifikiria Algeria, namkumbuka babu yangu. Tangu utoto wangu, nimekuwa na utamaduni wa Kialgeria katika familia," amesema na kuongeza. "Nilizungumza naye kabla ya kuchezea timu ya taifa, alifurahi kwa uamuzi huu. Kila wakati nilipoitwa kwenye timu ya taifa, amekuwa akinipigia na nilifanya uamuzi ambao anajivunia sana."
Na baba yake mzazi naye amesapoti uamuzi wa mtoto, ambapo Luca amesema: "Ananisapoti. Aliniambia, kuwa makini, huu ni uamuzi wako. Nakupa ushauri, lakini mwisho wa yote uamuzi ni wako. Na hapo, baada ya kocha na rais wa shirikisho kuwasiliana na mimi, nilikuwa tayari kwenda kuiwakilisha nchi yangu. Baada ya hapo, nilizungumza na familia yangu na walilifurahia jambo hilo."