Liverpool yamweka mezani kocha mwingine

LIVERPOOL,ENGLAND. LICHA ya ripoti kudai Kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim amefikia makubaliano ya kujiunga na Liverpool mwisho wa msimu huu, taarifa kutoka Daily Mail imefichua kuna jina lingine lipo mezani kwa mabosi wa Liverpool.

Jina hilo ni la kocha wa zamani wa Bayern Munich na Monaco, Niko Kovac ambaye kwa sasa yupo huru tangu aachane na Wolfsburg mwanzoni mwa msimu huu.

Liverpool kwa sasa ipo katika mazungumzo na makocha mbalimbali huku Ruben ndio akionekana kuwa na nafasi kubwa ya kuajiriwa.

Mabosi wa majogoo hawa wa Jiji la Liverpool wameanzisha mazungumzo na Kovac ni kuweka akiba ikiwa mambo yataenda vibaya kati yao na Amorim.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka England, wawakilishi wa Kovac walikuwa jijini London katika siku za hivi karibuni na walikuwa wakifanya mazungumzo na baadhi ya timu za Ligi Kuu England kwa ajili ya kumtafutia ajira mteja wao na Liverpool ni moja kati ya timu ambazo ilizungumza nayo.

Kovac mwenye umri wa miaka 52 ni mzaliwa wa  Berlin Ujerumani lakini alikuwa akiitumikia timu ya taifa ya Croatia na alikuwa ni nahodha wao kabla ya kustaafu.

Akiwa kama kocha alishinda taji la German Cup akiwa na Eintracht Frankfurt mwaka 2018, kabla ya kushinda Ligi Kuu na German Cup akiwa na  Bayern Munich mwaka mmoja baada, baada ya hapo alienda kuifundisha AS Monaco mwaka 2020 hadi 2022, alipotimkia zake Wolfsburg na mambo yalikuwa magumu na akafungashiwa virago Machi mwaka huu.