Liverpool yaanza mkakati wa kumbakiza Mo Salah

Muktasari:

  • Taarifa ya Liverpool kutaka kuanza mazungumzo na staa huyo zimeibuka ikiwa ni siku kadhaa tangu aseme hadharani kwamba huu huenda ukawa msimu wake wa mwisho klabuni hapo kwani timu hiyo haijafanya mazungumzo yoyote na wawakilishi wake.

LIVERPOOL ina mpango wa kuanza mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji raia wa Misri, Mohamed Salah kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya.


Taarifa ya Liverpool kutaka kuanza mazungumzo na staa huyo zimeibuka ikiwa ni siku kadhaa tangu aseme hadharani kwamba huu huenda ukawa msimu wake wa mwisho klabuni hapo kwani timu hiyo haijafanya mazungumzo yoyote na wawakilishi wake.


Salah anayewindwa na timu mbalimbali za Saudi Arabia mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu na kulikuwa na taarifa kwamba hana mpango wa kusaini tena, badala yake anataka kuondoka.


Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Al Ittihad ya Saudi Arabia ilimpa supastaa huyo ofa ya mshahara unaofikia Pauni 100 milioni kwa mwaka ili akubali kujiunga nayo. Ikiwa Liverpool itafanikiwa kumshawishi Salah kuna uwezekano mkubwa ikamwongezea mshahara zaidi ya ule anaoupokea sasa.

CHELSEA ipo tayari kumuachia beki raia wa England, Ben Chilwell, 27, kwenda kwa mkopo Uturuki, lakini hadi sasa haijapokea ofa kwa timu yoyote iliyo tayari kumchukua. Chilwell ambaye alitajwa sana kwamba anaweza akajiunga na Manchester United katika dirisha la majira ya kiangazi, kuna uwezekano mkubwa akatimkia ama Uholanzi au Uturuki dirisha lijalo la Januari, 2025.

MAZUNGUMZO kati ya Chelsea na AEK Athens juu ya mshambuliaji wa matajiri hao wa Jiji la London, David Fofana, 21, yanaendelea na yanadaiwa kufikia katika hatua nzuri. Nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ni mmoja kati ya mastaa ambao Chelsea imewaondoa katika kikosi cha kwanza kwa msimu huu na kuwaambia watafute timu za kucheza.

GALATASARAY ipo katika mazungumzo na  Manchester United kwa ajili ya kumsajili kiungo Carlos Henrique Casimiro, 32, maarufu Casemiro kwa mkopo katika dirisha hili. Man United inadaiwa kuwa tayari kumuuza Casemiro baada ya kutoridhishwa na kiwango alichoonyesha katika mechi kadhaa za mwanzo wa msimu hususani dhidi ya Liverpool.

WEST Ham United inataka kumsajili beki wa zamani wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Mats Hummels, 35, ambapo ni mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika. Hummels ambaye msimu uliopita alicheza mechi 40 za michuano yote, amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali Ulaya tangu dirisha lililomalizika hivi karibuni.

REAL Betis ambayo iliwasilisha ofa ya kutaka kumsajili kiungo wa Manchester United na Denmark, Christian Eriksen katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi huenda ikarudi tena dirisha la majira ya baridi mwakani. Eriksen aliyedaiwa kuwa anauzwa katika dirisha lililopita, mpango huo umesitishwa baada ya Mason Mount kupata majeraha.

WINGA wa zamani wa Manchester United, Anthony Martial, 28, amepokea ofa kutoka AEK Athens ya Ugiriki ambayo ipo tayari kumpa mshahara utakaomfanya kuwa mchezaji anayepokea mkwanja mkubwa zaidi katika timu hiyo. Martial ambaye kwa sasa yupo huru alimaliza mkataba wake na Manchester United msimu uliopita na kwa muda sasa wawakilishi wake wanapokea ofa kutoka ligi ambazo hazijafunga usajili.

KIUNGO wa zamani wa Liverpool, Naby Keita, 29, ambaye kwa sasa anaitumikia Werder Bremen yupo katika mazungumzo na Istanbul Basaksehir  ya Uturuki kwa ajili ya kujiunga nayo siku chache zijazo baada ya dili lake la kujiunga na Sunderland kufeli kutokana kutofikia mwafaka juu ya maslahi binafsi. Mkataba wa sasa wa Keita na Bremen unamalizika 2026.