Liverpool yaanza mazungumzo na Andoni Iraola
Muktasari:
- Kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Aston Villa kimeiweka Liverpool katika hatari kubwa ya kukosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya ( UEFA Champions League) kuelekea mechi ya mwisho ya msimu.
LIVERPOOL, ENGLAND: Klabu ya Liverpool imeripotiwa kuanza mazungumzo ya siri na Kocha Mkuu wa Bournemouth, Andoni Iraola, huku mustakabali wa Arne Slot ndani ya Anfield ukiwa shakani baada ya msimu wa Ligi Kuu England.
Kipigo cha mabao 4-2 dhidi ya Aston Villa kimeiweka Liverpool katika hatari kubwa ya kukosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya ( UEFA Champions League) kuelekea mechi ya mwisho ya msimu.
Shinikizo limeongezeka zaidi kwa Slot (47) baada ya mshambuliaji tegemeo, Mohamed Salah, kuposti ujumbe mzito na wenye utata kwenye mitandao ya kijamii unaoashiria kuondoka kwake klabuni hapo.
Mtandao wa FootMercato umeripoti kuwa viongozi wa Liverpool wanajipanga kumfuta kazi Slot baada ya kushindwa kutetea taji la Ligi Kuu ya EPL, licha ya kutumia mamilioni ya pesa kusajili wachezaji wapya msimu uliopita.
Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool, Richard Hughes, anatajwa kuongoza mazungumzo hayo ya siri. Hughes ana uhusiano mzuri na Iraola (43) kwani ndiye aliyemleta Bournemouth wakati akiiongoza wa klabu hiyo ya ‘The Cherries’.
Liverpool inaamini hii ni fursa dhahabu kwani Iraola tayari ameshachukua uamuzi ya kuondoka Bournemouth mwishoni mwa msimu huu.
Mabosi wa Anfield wamevutiwa sana na mfumo wa uchezaji wa kocha huyo raia wa Hispania. Iraola ameshangaza wengi kwa kuifanikisha Bournemouth kufuzu michuano ya Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, licha ya kupoteza wachezaji nyota watano ndani ya miezi 12 iliyopita akiwemo beki Milos Kerkez aliyesajiliwa na Liverpool kwa Pauni 40 milioni.
Liverpool inakabiliwa na ushindani mkali kupata saini kocha huyo ambaye aliwahi kuinoa Rayo Vallecano ya kwao Hispania. Vilabu vingine vikiwemo Crystal Palace (ambapo Oliver Glasner anajiandaa kuondoka) pamoja na timu kadhaa za nje ya England zinamtamani Iraola.
Hapo awali, Xabi Alonso alikuwa kwenye rada za Liverpool, lakini alichagua kwenda kuchukua mikoba ya kuifundisha Chelsea, hatua iliyomfanya Iraola kupewa kipaumbele kwenye klabu ya Liverpool kwa sasa.
Ili kujinusuru kufukuzwa kazi, Arne Slot anapaswa kuiongoza Liverpool kupata ushindi wa pointi tatu dhidi ya Brentford katika mchezo wa mwisho wa msimu keshokutwa Jumapili.
Ushindi huo utawahakikishia nafasi ya tano bora na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ripoti zinasema kuwa kushindwa kufikia lengo hilo kutamaanisha mwisho wa kibarua chake.