Arne Slot akalia kuti kavu Liverpool
Muktasari:
- Wakati taarifa hizo zikiibuka, hivi karibuni ilielezwa wamiliki wa klabu hiyo, Fenway Sports Group, walikuwa wanamuunga mkono kocha huyo na kumpa nafasi ya kuendelea msimu mwingine.
TAARIFA zinasema kwamba, Liverpool inadaiwa kufikia uamuzi wa kumfuta kazi Arne Slot baada ya mashauriano na wachezaji wakubwa wa timu hiyo, kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na sakata hilo.
Msimu huu umeelezwa kuwa mbaya kwa Liverpool, huku Slot akionekana kushindwa kuleta mabadiliko chanya au kuhamasisha timu kwa kiwango kinachotakiwa baada ya msimu uliopita kuipa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL).
Wakati taarifa hizo zikiibuka, hivi karibuni ilielezwa wamiliki wa klabu hiyo, Fenway Sports Group, walikuwa wanamuunga mkono kocha huyo na kumpa nafasi ya kuendelea msimu mwingine.
Lakini kutokana na kuongezeka kwa ukosoaji kutoka kwa mashabiki, wanahabari na hata baadhi ya wachezaji, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Graeme Bailey, ameiambia TEAMtalk kwamba viongozi wa Liverpool wamebadili msimamo wao.
Bailey amesema viongozi ndani ya Liverpool wameanza kuwa na mashaka makubwa na sasa wanazingatia kwa uzito kumfuta kazi Slot.
“Michael Edwards na Richard Hughes wana mambo mengi ya kufikiria na kujadili,” Bailey ameeleza.
“Hali inayomhusu Slot inaendelea kuwa mbaya kwa kasi na ninaweza kusema kwamba si kila mtu ndani ya klabu anaamini kuwa anapaswa kubaki.
“Liverpool si klabu inayofanya uamuzi kwa hisia au papara, lakini umiliki wa klabu unatambua kabisa kuwa hali hii inaanza kuwa ya kutia wasiwasi mkubwa.
“Ninaambiwa kauli za Salah zimegusa wengi ndani ya klabu. Kwa ndani, kuna watu wengi wanaomuunga mkono kuhusu alichosema na wanaelewa kwa nini alitoa malalamiko hayo.”
Mwingine aliyeziibua taarifa hizo ni Chris Royce, ambaye amesema Slot hataendelea kuwa kocha wa Liverpool kwa msimu ujao licha ya bodi ya klabu hapo awali kuamua kumpa muda zaidi kocha huyo wa Uholanzi.
Slot (47), alitua Liverpool msimu uliopita 2024–2025 na kuipa timu hiyo taji la Ligi Kuu England akichukua mikoba ya Jürgen Klopp.
Mafanikio hayo yalimfanya kutangazwa kuwa Kocha Bora wa Msimu Premier League 2024–2025 sambamba na tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka kutoka Chama cha Makocha England. Pia msimu huo alikuwa Kocha Bora wa Mwezi November 2024, kisha msimu huu akabeba tuzo hiyo Agosti 2025.