Liverpool yaangukiwa na bahati ya ubingwa EPL
Muktasari:
- Vinara hao wa Ligi Kuu England ilionekana kama wapo kwenye wakati mzuri baada ya kuongoza 2-0 uwanjani Anfield, lakini Wolves ilipambana na kupata bao moja, ambalo liliibua wasiwasi mkubwa kwa kocha Arne Slot.
LONDON, ENGLAND: LIVERPOOL imepewa asilimia 87.65 ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu licha ya kushinda kwa mbinde dhidi ya Wolves, Jumapili.
Vinara hao wa Ligi Kuu England ilionekana kama wapo kwenye wakati mzuri baada ya kuongoza 2-0 uwanjani Anfield, lakini Wolves ilipambana na kupata bao moja, ambalo liliibua wasiwasi mkubwa kwa kocha Arne Slot.
Liverpool ilishuhudia pengo la pointi kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo likipungua baada ya Arsenal kuichapa Leicester City, Jumamosi na kufanya kubaki pointi nne. Liverpool ilirejesha uongozi wake wa pointi saba baada ya ushindi dhidi ya Wolves.
Kwa mujibu wa Opta, Arsenal imepewa asilimia 12.35 ya kushinda taji hilo, licha ya kutabiriwa itamaliza ligi ikiwa na pointi 80, wakati Liverpool imetabiriwa itamaliza na pointi 87.
Macho ya wengi yanasubiri mechi ya miamba hiyo miwili kwenye mbio za ubingwa zitakapochuana zenyewe uwanjani Anfield, Mei. Kabla ya mechi hiyo, kila timu itakabiliwa na mechi ngumu na Liverpool watakuwa na kasheshe la kuikabili Manchester City ugenini.
Kwa Arsenal, shughuli pevu kwenye mechi zijazo ni ile pia ya kuikabili Nottingham Forest ugenini, ikiwa kwenye mchakamchaka wa vuta vikuvute kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.