Liverpool yaandamwa na majeruhi kibao
Muktasari:
- Beki huyo wa pembeni alilazimika kutolewa nje dakika nne tu baada ya kuanza kwa mchezo wa mwisho wa hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi.
LIVERPOOL, ENGLAND: IDADI ya mastaa wanaosumbuliwa na majeraha katika kikosi cha Liverpool imezidi kuongezeka baada ya Jeremie Frimpong kupata jeraha la nyama za nyuma ya paja (hamstring) katika mechi dhidi ya Qarabag, katikati ya wiki hii.
Beki huyo wa pembeni alilazimika kutolewa nje dakika nne tu baada ya kuanza kwa mchezo wa mwisho wa hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi.
Frimpong, 25, alianguka chini baada ya kukimbilia mpira na alionekana kukunja uso kutokana na maumivu ya mguu wake.
Huyu anakuwa ni mchezaji wa tatu wa Liverpool kupata jeraha la nyama za paja msimu huu na inaelezwa anaweza kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Mchezaji mwenzake Dominik Szoboszlai alitambua haraka ukubwa wa jeraha hilo na akawa anaonyesha ishara kwa benchi la ufundi hawezi kuendelea.
Hadi sasa Liverpool inawakosa mastaa wake, Joe Gomez, Conor Bradley na Ibrahima Konate.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya majeraha ya Gomez na Konate, Slot alisema mastaa hao wanaweza kurejea Kiwanjani hivi karibuni.
Gomez aliumia alipokuwa akijaribu kuzuia bao katika kipigo cha 3-2 dhidi ya Bournemouth Jumamosi.
Jeraha la Frimpong halikuvuruga jitihada za Liverpool, kwani iliibamiza Qarabag mabao sita na kufuzu kwenda hatua ya 16 bora.
Mashabiki wa Liverpool walionekana kuumizwa sana na jeraha hilo na walitoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii na mmoja aliandika: "Nani ametulaani msimu huu, ndilo swali tunalopaswa kujiuliza.”
Mwingine akasema: “Alikuwa mchezaji anayepata majeraha mara kwa mara, usajili wa majira ya kiangazi yaliyopita ulikuwa wa ovyo sana."