Liverpool, United zadaiwa kutuma ofa kumpata Yoro

Muktasari:

  • Staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa akihusishwa sana na Manchester United na Liverpool, hivyo kuna uwezekano ofa hiyo ikawa imetoka kwa moja kati ya timu hizo.

LILLE imekataa ofa ya Pauni 42.3 milioni kutoka kwa moja kati ya timu zinazohitaji huduma ya beki wao wa kati Leny Yoro katika dirisha hili, imeelezwa.

Staa huyu wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa akihusishwa sana na Manchester United na Liverpool, hivyo kuna uwezekano ofa hiyo ikawa imetoka kwa moja kati ya timu hizo.

Leny mwenyewe anaripotiwa kupendelea zaidi kujiunga na Real Madrid na ikishindikana ndio ataangalia timu nyingine.

Inaelezwa Lille imepandisha bei ya fundi huyu baada ya kuona timu nyingi kubwa zinataka kumsajili.

Hapo awali ripoti zilieleza kwamba Yoro anaweza akauzwa hata kwa Pauni 40 milioni wakati ambao Liverpool na Man United ndio zilionekana kuwa timu pekee zinazomhitaji.

Hata hivyo, uwepo wa Madrid kwenye dili umeifanya Lille ihitaji zaidi ya Pauni 50 milioni.

Mkataba wa staa huyu unamalizika mwaka 2025.

Man United imedhamiria kujiimarisha baada ya kuwa na msimu mbaya uliomalizika kwenye ligi, ingawa ilijitutumua mwishoni na kushinda Kombe la FA.