Liverpool mstari wa mbele dili la Anthony Gordon
Muktasari:
Gordon amekuwa kwenye kiwango bora kwa misimu kadhaa akiwa na Newcastle na msimu huu amecheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao 10.
LIVERPOOL ipo mbele katika mbio za kumsajili winga wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Anthony Gordon, 24, ambaye pia anahitajika na Manchester City na Arsenal.
Hata hivyo, dili hilo halitakuwa rahisi kwani Newcastle inahitaji takribani Pauni 95 milioni, kiasi ambacho kinaonekana kuwa kikubwa kwa timu hizo zinazomhitaji.
Gordon amekuwa kwenye kiwango bora kwa misimu kadhaa akiwa na Newcastle na msimu huu amecheza mechi 35 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Newcastle haina mpango wa kupunguza bei yake kwani hakuna presha ya kumuuza kwa sasa ikizingatiwa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika timu yao. Liverpool inahitaji huduma ya staa huyu kwa ajili ya kuboresha eneo lao la ushambuliaji ambalo linaonekana kuwa na madhaifu mengi kwa msimu huu kiasi cha kusababisha waanze ligi na kushindwa kuwa katika mbio za ubingwa wa kutetea taji lao.
Gordon mwenyewe hana mpango wa kulazimisha kuondoka na atasubiri hadi timu zitakapofikia mwafaka kwani anaona hakuna shida akiendelea kubakia Newcastle na hakuna shida pia akiondoka.
Mohamed Salah
TAARIFA za ndani zinadai kuna mazungumzo ya siri yanaendelea baina ya wawakilishi wa mshambuliaji wa Liverpool na mabosi wa majogoo hao ikiwa ni sehemu ya kutaka mshambuliaji huyo kutimkia Saudi Arabia katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Salah ambaye ana mkataba na Liverpool hadi mwaka 2027, anatajwa kuwa na asilimia kubwa za kuondoka katika dirisha lijalo kwa ajili ya kutafuta changamoto baada ya kudumu Anfield kwa zaidi ya miaka saba.
Kuondoka kwa Salah kumelazimisha Liverpool kuanza harakati za kutafuta mshambuliaji wa kuziba pengo lake.
Mateus Mane
MANCHESTER United ipo katika vita kali dhidi ya Liverpool, kwa ajili ya kuiwania saini ya mshambuliaji chipukizi wa Wolverhampton Wanderers, Mateus Mane mwenye umri wa miaka 18.
Mane, ambaye amezaliwa Ureno lakini anachezea timu za vijana ya England, anaonekana kuwa na kipaji kikubwa na timu nyingi zimevutiwa naye.
Wolves inahitaji takribani Pauni 50 milioni kwa ajili ya kumuuza kwani inaamini ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kusaidia sana timu siku za usoni ikiwa atabaki. Mkataba wake wa saa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Lucas Bergvall
TOTTENHAM Hotspur imekataa rasmi maombi kutoka Aston Villa na Chelsea yaliyowasilishwa mwezi uliopita yakitaka kumsajili kiungo wao wa kimataifa wa Sweden, Lucas Bergvall, 20.
Bergvall anaonekana kuwa sehemu muhimu ya mipango ya muda mrefu ya Spurs, baada ya kuonyesha kiwango bora tangu ajiunge na klabu hiyo.
Viongozi wa Spurs wanataka kusubiri walau kwa msimu mmoja au miwili kabla ya kumuuza wakiamini wakati huo watapata pesa nyingi zaidi tofauti na ilivyo saa. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2031.
Castello Lukeba
KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amewaambia mabosi wake juu ya dhamira yake ya kumsajili beki wa kati wa kimataifa wa Ufaransa, Castello Lukeba, 23, kutoka RB Leipzig.
Leipzig wako tayari kumuachia kwa ada ya uhamisho itakayokuwa chini ya takribani Pauni 52.1 milioni, na Arteta anamtamani sana kwa sababu anaona ana sifa zinazomfaa kikamilifu katika falsafa yake ya soka.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Lukeba amecheza mechi 19 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Antonio Nusa
ARSENAL imetuma maskauti wake kwenda Ujerumani kwa ajili ya kumchunguza winga wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Norway, Antonio Nusa, 20.
Nusa, ambaye amekuwa akionyesha kiwango bora tangu mwaka jana, amekuwa akifuatiliwa na timu nyingi zinazodai kwamba zinaweza kuwasilisha ofa rasmi ifikapo mwisho wa msimu huu.
Nusa mwenyewe anatamani sana kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi akiamini kuwa huu ndio wakati wake.
James Trafford
ASTON VILLA imeanza mipango ya kumtafuta mrithi wa kipa wake namba moja, Emiliano Martinez, 33, anayetarajiwa kuondoka katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kipa wa Manchester City na timu ya taifa ya England, James Trafford, 23, ndio anatajwa kuwa katika rada zao.
Trafford ambaye kwa sasa anahudumu kama kipa namba mbili katika kikosi cha Man City ameonyesha kutamani sana kuondoka ili apate nafasi ya kuwa namba moja.
Martinez amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa kubwa barani Ulaya na Saudi Arabia.
Federico Dimarco
MANCHESTER United imetuma maskauti wake kwenda Italia, Jumamosi iliyopita kushuhudia mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa San Siro kwa ajili ya kutazama wachezaji wawili inaowahitaji.
Mastaa hao wawili ni beki wa kushoto wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Federico Dimarco, 28, pamoja na beki wa kati wa Juventus, Pierre Kalulu, 25.
Dimarco amekuwa katika kiwango bora msimu huu, sawa na Kalulu ambaye Juventus hawapo tayari kumuuza kirahisi isipokuwa kwa ofa nono.Man United inataka kuimarisha safu ya ulinzi kuelekea msimu ujao.