Liverpool kuilipa fidia Chelsea
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo, 17, alijiunga na Liverpool, Septemba 2024 baada ya kuondoka akademi ya Chelsea, jambo linalowapa The Blues haki ya kupata fidia.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeamriwa kuilipa Chelsea Pauni 2.8 milioni baada ya baraza la usuluhishi kutoa uamuzi kuhusu usajili wa Rio Ngumoha.
Mshambuliaji huyo, 17, alijiunga na Liverpool, Septemba 2024 baada ya kuondoka akademi ya Chelsea, jambo linalowapa The Blues haki ya kupata fidia.
Inaripotiwa kuwa Chelsea walikasirishwa sana na kuondoka kwa Ngumoha kwenda Liverpool, kwani walitambua kuwa ni kipaji cha kipekee na walikuwa wamempa mikataba kadhaa wakijaribu kumbakisha.
Uamuzi wake wa kukataa dili lao na kuelekea Merseyside ulizidisha mvutano kati ya vigogo hao wawili wa Ligi Kuu England.
Imeelezwa pia kuwa Chelsea walizuia skauti wa vijana wa Liverpool kuhudhuria mechi za akademi kama hatua ya kujibu kuondoka kwa Ngumoha.
Alikuwa na umri wa miaka 16 alipojiunga na Liverpool kwa mazingira yaliyozua mabishano, hali iliyopelekea kesi hiyo kufikishwa kwenye baraza la PFCC.
Baraza hilo lilihitajika ili kubaini kiasi cha fedha ambacho Chelsea inastahili kulipwa kwa mchango wao kumkuza Ngumoha. Kwa mujibu wa The Athletic, uamuzi huo ambao hauwezi kujadiliwa tayari umefahamishwa kwa klabu zote mbli.
Liverpool watalazimika kuilipa Chelsea ada ya awali ya Pauni 2.8 milioni, kiasi ambacho kinaweza kuongezeka kwa kiwango kikubwa endapo masharti mengine yatatimia.
Kiasi hicho kinaweza kufikia Pauni 6.8 milioni iwapo vigezo fulani vitafikiwa, vikiwemo kucheza timu ya wakubwa, mikataba na kuitwa timu ya taifa. Aidha, Chelsea itapata asilimia 20 ya faida endapo Ngumoha atauzwa kwenda klabu nyingine.
Ngumoha tayari ameing’ara katika timu za vijana za England na sasa anachezea chini ya miaka 19, ambacho tayari amecheza mechi nane na kufunga bao moja.
Tangu alipoanza kuchezea timu ya kwanza ya Liverpool chini ya kocha Arne Slot Januari 2025, Ngumoha amecheza mechi 14, na kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza kwenye kikosi cha Liverpool katika Kombe la FA.
Alifunga bao la ushindi lisilosahaulika baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Newcastle Agosti mwaka jana na amekuwa akijumuishwa mara kwa mara katika kikosi cha Ligi Kuu England.
Akizungumzia Ngumoha, Slot amesema: “Nadhani ana dakika nyingi zaidi za kucheza kuliko mchezaji yeyote mwenye umri wa miaka 17 katika Ligi Kuu. Hilo linakuonyesha ni kwa kiasi gani anapata muda wa kucheza, na jinsi hilo lilivyo jambo la kipekee kwa mchezaji wa umri huo.”