Lionel Messi, Lewandowski, Mbappe waanza kazi Qatar

DOHA QATAR. QATAR kumenoga. Lionel Messi ataanza kazi rasmi. Robert Lewandowski ataamsha dude na Kylian Mbappe ana shughuli ya kuibeba Les Bleus. Mambo ni leo Jumanne.

Kuna mtu atachapwa, tema mate tumchape. Macho ya wengi na masikio yataelekezwa kwa supastaa Messi, ambapo mshindi huyo mara saba wa Ballon d’Or atacheza dansi lake la mwisho kwenye soka la dunia, wakati atakapoanza kazi kwenye Kundi C kwa kumenyana na Saudi Arabia. Supastaa mwingine kwenye Kundi C ni Lewandowski wa Poland, ambaye chama lake litakuwa na shughuli ya kuwakabili Mexico. Kwenye Kundi C, timu inayoonekana kuwa na udhaifu kidogo ni Saudi Arabia.

Argentina na Saudi Arabia zimewahi kukutana mara moja tu kwenye mechi ya kirafiki iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana, 2012. Lakini, kwa sasa miamba hiyo itakutana kwenye mechi ya ushindani, huku Messi na jeshi lake la Argentina akiwa na kazi moja ya kujaribu kusaka taji la Kombe la Dunia ambalo alikaribia kulibeba 2014, walipochapwa kwenye mchezo wa fainali ya Ujerumani huko Brazil.

Mchezo mwingine kwenye Kundi C, utazikutanisha Mexico na Poland. Kipute hicho ni biashara ya Lewandowski dhidi ya kipa hatari Guillermo Ochoa. Chama la Mexico lina mafundi wengi pia akiwamo Raul Jimenez wa Wolves, huku kwenye kikosi cha Poland staa mwingine tishio ni mshambuliaji Arkadiusz Milik na kipa Wojciech Szczesny.

Poland na Mexico zimekutana mara tatu kwenye mechi za kirafiki, ambapo Mexico ilishinda mara moja, huku mechi mbili zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 kila moja.

Maswali mengi yanayoulizwa ni kama Saudi Arabia wataweza kumudu shughuli ya kuwakabili Argentina yenye sura nyingi matata kabisa, akiwamo Angel Di Maria.

Mchakamchaka wa Kombe la Dunia 2022 utaendelea kwenye Kundi D, lenye timu za Ufaransa, Denmark, Australia na wawakilishi wa Afrika, Tunisia.

Karata ya kwanza kwenye kundi hilo, mabingwa watetezi Ufaransa wenye huduma ya Mbappe itakipiga na Austrailia, huku Denmark ya Christian Eriksen itakuwa na shughuli pevu mbele ya Waarabu wa Tunisia.

Kocha wa Les Bleus, Didier Deschamps anakuna kichwa baada ya kikosi chake kilichochukua ubingwa wa dunia miaka minne iliyopita, mastaa wake muhimu ikiwamo Paul Pogba na N’Golo Kante kukosekana huko Qatar kutokana na kuwa majeruhi, huku akiwapoteza pia washambuliaji wake Christopher Nkunku na Karim Benzema kuwa majeruhi. Lakini, Ufaransa ina watu makini akiwamo Antoine Griezmann na Ousmane Dembele. Wapinzani wao kwenye mechi ya kwanza, Australia, wameshawahi kukutana nao mara nne huko nyuma, ikiwamo mara moja kwenye makundi ya Kombe la Dunia 2018, ambapo Ufaransa ilishinda mabao 2-0. Mechi mbili zilikuwa za kirafiki, ambapo moja Ufaransa ilishinda 6-0 na nyingine ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, huku mchezo wa nne ulikuwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2001, Australia ilishida 1-0.

Shughuli nyingine kwenye Kundi D itawahusu Denmark na Tunisia. Timu hizo ziliwahi kukutana mara moja tu, kwenye mechi ya kirafiki 2002, ambapo Denmark ilishinda 2-1.

Macho ya wengi yatakuwa kwenye kikosi cha Denmark, kitakachokuwa na huduma ya Eriksen, mchezaji ambaye aliwahi kupatwa na tatizo la mshuko wa moyo na kuanguka uwanjani katika michuano ya Euro 2020. Lakini, sasa yupo fiti na atakuwapo Qatar.