Lionel Messi azidi kuweka rekodi
Muktasari:
- Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa staa huyu kushinda tuzo, baada ya mwaka jana kuikosa kwa mabao matatu tu dhidi ya Christian Benteke wa D.C. United.
FLORIDA, MAREKANI: STAA wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi ameweka rekodi baada ya kushinda tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Marekani , akimaliza msimu akiwa na mabao 29, akiwapiku Sam Surridge wa Nashville SC na Denis Bouanga wa LAFC, ambao wote walifunga mabao 24 kila mmoja.
Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa staa huyu kushinda tuzo, baada ya mwaka jana kuikosa kwa mabao matatu tu dhidi ya Christian Benteke wa D.C. United.
Messi ameandika historia kuwa mchezaji wa kwanza wa Inter Miami kushinda tuzo hiyo katika msimu wake wa pili, na pia amekuwa Muargentina wapili kufanya hivyo katika ligi hiyo baada ya Valentin Castellanos, ambaye alifunga mabao 19 akiwa na New York City FC mwaka 2021.
Mabao yake 29 pia yanamweka katika orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi katika historia ya ligi hiyo tangu mwaka 2005, akizidiwa na Josef Martinez (mabao 31 mwaka 2018) na Carlos Vela (mabao 34 mwaka 2019).
Messi pia ana wastani wa bao 1.03 kwa mechi, nyuma kidogo ya Vela aliye na wastani wa bao 1.10 aliyoiweka mwaka 2019.
Vilevile, Messi alifunga hat-trick yake ya kwanza ya msimu huu katika siku ya mwisho wa ligi na akaweka rekodi yakuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya ligi hiyo kufunga katika mechi 10 zenye mabao zaidi ya moja akiwavuka Stern John , Mamadou Diallo , na Zlatan Ibrahimovic ambao waliwahi kufanya hivyo katika mechi nane.
Kuhusika kwake katika mabao 48 (mabao 29 , asisti 19 ) msimu pia kumemfanua ashike nafasi ya pili ya kuhusika katika mabao mengi zaiid kwa msimu mmoja katika historia ya ligi hiyo akizidiwa na Carlos Vela aliyehusika katika mabao 49 mwaka 2019.