Ligi ya Mabingwa Ulaya, London imenoga
Muktasari:
- Timu hizi ambazo zipo katika nafasi ya saba na ya nane katika msimamo wa jumla wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kila moja ikiwa na pointi saba, zitakuwa zina kibarua cha kukusanya pointi zaidi ili kusogea katika nafasi za juu.
LONDON, ENGLAND: Ni siku ya kawaida pale London, mishale ya saa inasoma saa 2:00 usiku. Afrika Mashariki mshale wa saa unasoma saa 5:00 usiku. Ni kivumbi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea itakuwa mwenyeji wa Barcelona kwenye dimba la Stamford Bridge.
Timu hizi ambazo zipo katika nafasi ya saba na ya nane katika msimamo wa jumla wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kila moja ikiwa na pointi saba, zitakuwa zina kibarua cha kukusanya pointi zaidi ili kusogea katika nafasi za juu.
Hii itakuwa ni mechi ya kwanza kwa Chelsea kukutana na Barcelona katika mashindano yote tangu mwaka 2018 ambapo mara ya mwisho Barca iliibuka na ushindi.
Kabla ya mechi hiyo ya 2018 ambayo ilikuwa ni ya Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora, Chelsea haikuwa imepoteza mechi yoyote dhidi ya Barca tangu Februari 2006. Katika mechi nane sita zilimalizika kwa sare kisha mbili Chelsea ikashinda.
Timu yoyote kati ya hizi ikiwa itashinda mechi hii itasogea juu ya mwenzake na pengine kufika katika Top 5.
Mbali ya mechi hii ambayo inatarajiwa kuvutia watu wengi, kutakuwa pia na mechi nyingine nane zitakazopigwa katika maeneo mbalimbali.
England itashuhudiwa pia mechi ya Manchester City itakayoikaribisha Bayer Leverkusen inayoonekana kupitia nyakati ngumu tangu kuanza kwa msimu huu, mechi ikitarajiwa kuanza saa 5:00 usiku pia.
Newcastle United ambayo imesafiri hadi Ufaransa itakuwa na kazi ya kufanya mbele ya Marselle ambayo haina hali nzuri sana katika msimamo wa michuano hiyo.
Ikiwa Newcastle itashinda mechi hiyo inaweza kupanda hadi ndani ya Top 4 kutoka nafasi ya sita ambayo inaishikilia kwa sasa.
Mabingwa watetezi wa Serie A, Napoli wataikaribisha Qarabag FK kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Diego Armando Maradona wakati Juventus ikisafiri hadi Denmark kuumana na Bodo/Glimt.
Borussia Dortmund nayo itaikaribisha Villarreal huku Jose Mourinho na vijana wake wa Benfica wakiwa ndio wa kwanza kufungua dimba kwa mechi ya mapema wakicheza dhidi ya Ajax ugenini kuanzia saa 2:45 usiku.
Kiufupi viwanja vya Ulaya vitawaka moto wiki hii.