Ligi Kuu England ni mchakamchaka chinja!
Muktasari:
- Shughuli pevu itakuwa huko Emirates, wakati Arsenal itakapokuwa na mtihani wa kuwakabili mahasimu wao Tottenham Hotspur katika mechi ambayo itahitaji kushinda ili kuendelea kuweka hai pengo lake la pointi kwenye msimao wa ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND: ULE utamu wa Ligi Kuu England unarudi tena wikiendi hii, kila timu ikijaribu kusaka ushindi muhimu katika mchakamchaka wa ligi hiyo yenye ubabe mwingi.
Shughuli pevu itakuwa huko Emirates, wakati Arsenal itakapokuwa na mtihani wa kuwakabili mahasimu wao Tottenham Hotspur katika mechi ambayo itahitaji kushinda ili kuendelea kuweka hai pengo lake la pointi kwenye msimao wa ligi hiyo.
Msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma kwa sasa, Arsenal inaongoza kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya timu inayoshika namba mbili, Manchester City. Arsenal imekusanya pointi 26 katika mechi 11, wakati Man City imekuwanya pointi 22 katika idadi kama hiyo ya mechi.
Ubaya ni kwamba Arsenal itaingia uwanjani kukabiliana na Spurs, Jumapili, wakati mpinzani anayekimbia katika vita hiyo ya kukaa kileleni, Man City, yenyewe itarusha kete yake muhimu Jumamosi.
Hata hivyo, Man City yenyewe pia haitakuwa na kibarua chepesi, ambapo itakwenda huko St James’ Park kukipiga na Newcastle United. Ni mechi ya kibabe.
Ushindi kwa Man City utapunguza pengo la pointi kubaki kuwa moja tu, kitu ambacho kinaweza kuipa presha kubwa Arsenal kabla ya mechi yao ya kuikabili Spurs.
Rekodi zinaonyesha kwamba Man City na Newcastle United kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara 50, huku mara 10 mechi zao zilimalizika kwa sare. Katika mechi hizo, Newcastle imeshinda nane tu, mara saba nyumbani na moja tu ilipokwenda ugenini.
Man City yenyewe imeshinda mara 32, mara 12 ilipokwenda kucheza uwanjani St James’ Park, huku mara 20 ilishinda kwenye uwanja wake wa nyumbani katika mechi zake ilizocheza dhidi ya Newcastle. Hivyo, katika kipute hicho cha St James’ Park, Man City itakwenda ikiwa na nafasi kubwa ya kushinda kutokana na rekodi zinavyosoma timu hizo zilipokutana.
Kwa upande wa Arsenal, rekodi za mechi zao dhidi ya Spurs kwenye Ligi Kuu England ni 66 zilizofanyika hadi sasa, ambapo mara 24 zilimalizika kwa timu hizo kutoa sare, huku Arsenal ikionyesha ubabe kwa kushinda mara 27 dhidi ya 15 ilizoshinda Spurs. Katika ushindi huo wa Arsenal, mara 19 ilifanya kwenye mechi ilizocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani na nane tu ugenini, wakati Spurs yenyewe imeshinda mara 13 nyumbani na mbili tu ilipokwenda kuifuata Arsenal kwao. Vita ni kali.
Chelsea kwenye nafasi ya tatu, ikiwa nyuma kwa pointi sita nyuma ya vinara Arsenal, yenyewe itahitaji kushinda ili kupunguza pengo la pointi ili kubaki tatu kabla ya The Gunners haijacheza. Chelsea itakuwa na mchezo wa mapema Jumamosi, kumenyana na Burnley ugenini. Hiyo itakuwa mechi ya 19 kwa Burnley na Chelsea kumenyana kwenye Ligi Kuu England, huku mara 18 zilizopita, sare zilikuwa tano, huku The Blues ikishinda 12, mara nane ugenini na nne ilipocheza nyumbani.
Burnley yenyewe imeshuhudia ushindi mara moja tu na huo ulikuwa kwenye uwanja wa ugenini, hivyo mchana wa Jumamosi itashuka kwenye uwanja wake wa nyumbani kujaribu kusaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Chelsea kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
Mabingwa watetezi, Liverpool ambao wamekuwa na kipindi kigumu kwenye Ligi Kuu England msimu huu, itakuwa na shughuli pevu uwanjani Anfield kwa kumenyana na Nottingham Forest, ambayo pia inajitafuta ili kuwa sawa baada ya kufanya vibaya na kubadilika makocha mara kadhaa ndani ya msimu huu.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Forest na Liverpool zimekutana mara 16 katika mechi za Ligi Kuu England, ambapo sare ni tano, huku Liverpool ikishinda saba, mara sita nyumbani na moja ugenini, wakati Forest imeshinda nne, mara moja tu ugenini huko tatu ilishinda nyumbani.
Mashabiki wa Manchester United watalazimika kusubiri hadi Jumatatu kuishuhudia timu yao itakaposhuka uwanjani Old Trafford kukabiliana na Everton, ambayo imekuwa na kiwango kizuri sana kwenye ligi hiyo msimu huu. Namba zinaonyesha kwamba, Man United na Everton zimekutana mara 66 kwenye Ligi Kuu England, ambapo mara 14 mechi zake zilimalizika kwa sare, huku Man United ikishinda 42, mara 23 nyumbani na 19 ugenini, huku Everton ikipata ushindi mara 10, nane ilipocheza nyumbani na mbili tu ugenini. Je, hali itakuwaje safari hii?
Mchakamchaka wa ligi hiyo utashuhudia mechi nyingine kadhaa wikiendi hii, ambapo ukiweka kando kipute cha North London derby hiyo Jumapili, mechi nyingine itakayopigwa siku hiyo, itakuwa na kibabe sana, ambapo Leeds United itajimwaga kwenye uwanja wake wa nyumbani kukabiliana na Aston Villa, ambayo siku zote imekuwa ikichuana kutafuta nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya tangu ilipoanza kuwa chini ya Mhispaniola, Unai Emery.
Vipute vya Jumamosi, vitashuhudia, Wolves ikikipiga na Crystal Palace, Fulham na Sunderland, ambayo imekuwa moto kwelikweli msimu huu, huku Brighton ikicheza na Brentford na Bournemouth ikimaliza ubishi na West Ham United katika mechi nyingine inayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa katika ligi hiyo.