Palmer majanga! Kuzikosa Barcelona, Arsenal baada ya kuvunjika kidole
Muktasari:
- Palmer alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu japo alishaungana na wenzake kwa mazoezi, lakini majanga mengine yamempata kwa kuvunjika kidole akiwa nyumbani.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amekiri Cole Palmer amepata jeraha jingine jipya kabla ya safari ya Jumamosi kwenda Burnley katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL).
Palmer alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu japo alishaungana na wenzake kwa mazoezi, lakini majanga mengine yamempata kwa kuvunjika kidole akiwa nyumbani.
Ushindi kwenye Uwanja wa Turf Moor unaweza kuipeleka Chelsea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England. Hata hivyo, katika mkutano wa waandishi wa habari wa asubuhi ya leo, Ijumaa, Maresca amethibitisha pigo jipya kwa Palmer.
Kulikuwa na matumaini kiungo huyo wa England angepona na kuwahi mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona wiki ijayo, lakini Maresca amesema: “Inawezekana hatakuwa tayari kwa kesho, Barcelona kwa hakika hapana, Arsenal pia hapana. Kwa bahati mbaya alipata ajali nyumbani na kidole chake. Lakini si kitu kikubwa. Hakika hatarudi wiki ijayo.”
“Hatuna uhakika. Kidole kimevunjika. Tunachojua ni kwamba hatapatikana wiki hii na wiki ijayo,” amesema Maresca na alipoulizwa kilichosababisha tukio hilo, Maresca ameeleza:
“Mimi mwenyewe naamka usiku mara kadhaa kwenda chooni, napiga kichwa, mguu, kila kitu, inaweza kutokea kwa mtu yeyote."
Mara ya mwisho kumwona ilikuwa jana asubuhi akiwa hana soksi, hana kandambili, hana chochote. Sijui leo yuko vipi. Ilikuwa chumbani mwa kubadilishia nguo. Hakuwa anachechemea, alionekana sawa, lakini ni kidole kidogo cha mguu, kinaweza kuwa chenye maumivu.”
Alipoulizwa kama Chelsea inaweza kufanikiwa bila kiungo mshambuliaji Maresca amejibu: “Hapana kabisa, sifikirii hivyo. Timu inapendelea Cole akicheza, nami najisikia vizuri zaidi akiwa uwanjani. Lakini asipokuwepo, tunahitaji kutafuta mbinu mbadala. Timu inafanya vizuri, vizuri sana. Kwa kocha yeyote, ni vizuri kuona timu inaendelea vizuri hata kama mchezaji muhimu anakosekana.”
Kuhusu anachotarajia kutoka kwa Burnley, Maresca anaamini itakuwa mechi tofauti kabisa na ile waliyoishinda dhidi ya Wolves kabla ya mapumziko ya kimataifa.
“Itakuwa mechi tofauti. Kesho, tunahitaji kutumia mkakati na mbinu tofauti. Itakuwa mechi ngumu baada ya mapumziko ya kimataifa, saa 6:30 mchana, ugenini, kila mara huwa ngumu,” amesema Maresca.
Maresca pia aliulizwa kuhusu kurejeshwa kwa mshangao kwa beki Axel Disasi kwenye kikosi cha wakubwa. Mfaransa huyo alikuwa ametengwa tangu maandalizi ya msimu, lakini sasa amerudi kufanya mazoezi na benchi la ufundi.
Kocha amefafanua: “Nimesema mara nyingi kuwa Axel na Raheem (Sterling) ni wachezaji wa Chelsea. Axel anasaidia timu ya pili, wachezaji vijana. Tulikuwa na wachezaji watano au sita wakati wa mapumziko na Axel alikuwa sehemu ya baadhi ya mazoezi na timu ya pili, lakini nafikiri ni mazoezi moja tu. Kwa sasa anasaidia timu ya pili. Ni mchezaji wa Chelsea na yuko na timu ya pili.”
Kuhusu uvumi kwamba kipa Filip Jorgensen anapanga kuondoka Januari, Maresca amemalizia: “Nilizungumza na Filip mwanzoni mwa msimu na sikuongea naye siku za karibuni kuhusu hilo. Wachezaji wote wanaokosa muda wa kucheza wanataka kupata dakika zaidi, hilo ni jambo la kawaida kabisa.”