Leroy Sane katika anga za Arsenal

Muktasari:
- Sane ambaye msimu huu aliwahi kuweka wazi kwamba yupo tayari kurejea tena England, anadaiwa pia huenda akasaini mkataba mpya wa kubakia Bayern baada ya timu hiyo kuanza mazungumzo na wawakilishi wake.
ARSENAL imepanga kumsajili winga wa Bayern Munich na Ujerumani, Leroy Sane, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo atakuwa mchezaji huru kwani mkataba wake utakuwa unamalizika.
Sane ambaye msimu huu aliwahi kuweka wazi kwamba yupo tayari kurejea tena England, anadaiwa pia huenda akasaini mkataba mpya wa kubakia Bayern baada ya timu hiyo kuanza mazungumzo na wawakilishi wake.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Sane amecheza mechi 34 za michuano yote, amefunga mabao manane na kutoa asisti nne akiwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo.
Mbali ya Arsenal baadhi ya timu nyingine kubwa zinazohusishwa na staa huyu ni pamoja na Barcelona ambayo imeshawishika zaidi kutokana na hali ya mkataba wake.
Bruno Guimaraes
MKURUGENZI mpya wa mpira wa Arsenal, Andrea Berta anayetarajiwa kutangazwa hivi karibuni anadaiwa kuwa miongoni mwa wachezaji anaoweza kuwasajili baada ya kuanza kazi klabuni hapo ni kiungo wa Brazil anayeichezea Newcastle United, Bruno Guimaraes, pamoja na kiungo wa Real Sociedad na Hispania Martin Zubimendi, 26. Bruno Guimares ni mtu wa kazi sana na anazivutia klabu nyingi za England.
Jorrel Hato
LIVERPOOL imetuma maskauti wake kwenda Uholanzi kwa ajili ya kumtazama beki wa kushoto wa Ajax, Jorrel Hato, mwenye umri wa miaka 19, ambaye amecheza mara tano katika kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi.
Hato ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote.
Liverpool imekuwa ikiwanasa mastaa kadhaa wa Kiholanzi wanaofanya vyema kikosini humo.
Jeremie Frimpong
MANCHESTER City, Manchester United, Barcelona na Real Madrid zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya beki wa Bayer Leverkusen na Uholanzi, Jeremie Frimpong, mwenye umri wa miaka 24.
Frimpong ambaye alikuwa akiwindwa tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu huu amecheza mechi 39 za michuano yote.
Sean Longstaff
EVERTON imepanga kumsajili kiungo wa Newcastle United, Sean Longstaff, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo Sean mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kujiunga nao kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Newcastle.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Adam Wharton
MANCHESTER City ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo yao na Crystal Palace ili kumsajili kiungo wa timu hiyo, Adam Wharton, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Wharton amekuwa akihusishwa na Man City tangu dirisha la majira ya baridi mwaka jana ikielezwa kocha Pep Guardiola anamuona kama sehemu ya mipango yake ya muda mrefu.
Frenkie de Jong
BARCELONA imekataa ofa ya Pauni 57.8 milioni kutoka Manchester United iliyokuwa inahitaji saini ya kiungo wao raia wa Uholanzi, Frenkie de Jong, 27. De Jong ambaye tetesi za kuhusishwa kuondoka zimeanza dirisha lililopita la majira ya baridi baada ya kuripotiwa kwamba hana furaha ya kuendelea kusalia katika kikosi hicho, mkataba wake unamalizika mwakani.
Florian Wirtz
BAYER Leverkusen wana imani kubwa kwamba mchezaji wao wa kimataifa wa Ujerumani, Florian Wirtz, mwenye umri wa miaka 21, ataongeza mkataba wa kuendelea kusalia katika kikosi hicho licha ya timu nyingi kuhitaji kumsajili.
Bayern Munich na Manchester City ni kati ya timu zinazowinda saini yake.