Leicester kumtangaza Van Nistelrooy
Muktasari:
- Van Nistelrooy anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Steve Cooper, ambaye ametimuliwa klabuni hapo baada ya kudumu kwa siku 157 akiiongoza Leicester kucheza mechi 12 za Ligi Kuu ambapo ameshinda mechi mbili, ametoa sare mechi nne, akipoteza mechi sita na akivuna pointi 10 huku Leicester ikishika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi.
LEICESTER, ENGLAND: Leicester City inayoshiriki Ligi Kuu ya England huenda ikamtangaza aliyekuwa kocha msaidizi wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo.
Van Nistelrooy anatajwa kwenda kuchukua nafasi ya Steve Cooper, ambaye ametimuliwa klabuni hapo baada ya kudumu kwa siku 157 akiiongoza Leicester kucheza mechi 12 za Ligi Kuu ambapo ameshinda mechi mbili, ametoa sare mechi nne, akipoteza mechi sita na akivuna pointi 10 huku Leicester ikishika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi.
Kutimuliwa kwa Erik Ten Hag kwenye viunga vya United kulimfanya Van Nistelrooy kuwa kocha wa mpito wa United kabla ya ujio wa Ruben Amorim ambaye hakutaka kufanya kazi na staa huyo wa zamani.
Mshambuliaji huyo aliiongoza Man United kupata ushindi kwenye mechi tatu kati ya nne huku akitoa sare mechi moja ambapo mechi ya mwisho aliifunga Leicester mabao 3-0 kwenye Ligi Kuu.
Mholanzi huyo aliwahi kuwa kocha mkuu wa PSV ya Uholanzi ambapo aliiongoza kutwaa Kombe la Ligi msimu wa 2022-2023 kabla ya kujiunga na Man United kama kocha msaidizi wa Erik Ten Hag.
Ben Dowson ambaye alikuwa msaidizi wa Steve Cooper anatajwa kuiongoza Leicester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Brentford utakaopigwa kesho, Jumamosi kabla ya ujio wa Ruud Van.