Leicester City: Hadithi ya mafanikio yageuka funzo la uongozi mbovu
Muktasari:
- Ilikuwa ni hadithi ya kusisimua zaidi katika historia ya michezo. Lakini miaka kumi baadaye, hadithi hiyo ya kuvutia imegeuka kuwa fundisho chungu.
Mnamo Mei 2016, ulimwengu wa soka ulisimama. Leicester City, klabu ambayo msimu mmoja kabla ilikuwa inapambana kutoshuka daraja, ilitawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League).
Ilikuwa ni hadithi ya kusisimua zaidi katika historia ya michezo. Lakini miaka kumi baadaye, hadithi hiyo ya kuvutia imegeuka kuwa fundisho chungu.
The Foxes sasa wamezama rasmi kwenye dimbwi la (League One) daraja la tatu la soka nchini Uingereza.
Hali hii inathibitisha maneno ya kiungo Jordan James mnamo Desemba 2025, ambaye alionya kuwa yeyote aliyedhani klabu hiyo kubwa ingeweza kushuka daraja alikuwa "amepoteza akili."
Leo, ukweli huo mchungu umekuwa sehemu ya historia. Anguko la Leicester si ajali; ni matokeo ya mfululizo wa maamuzi mbovu, ubadhirifu wa fedha, na uongozi ulioshindwa kusoma alama za nyakati.
Mizizi ya mporomoko: Kosa la kwanza
Mporomoko huu haukuanza jana. Mbegu za dhoruba hii zilipandwa kati ya mwaka 2020 na 2022. Chini ya Brendan Rodgers, Leicester ilikuwa timu tishio, ikikaribia kumaliza katika nafasi nne za juu mara mbili mfululizo. Hata hivyo, mporomoko wa kiwango mwishoni mwa misimu hiyo uliwakosesha tiketi ya UEFA Champions League.
Kukosa mapato ya Champions League, kukiambatana na athari za kiuchumi za janga la Uviko-19, kuliwayumbisha wamiliki wa klabu hiyo raia wa Thailand, familia ya Srivaddhanaprabha.
Licha ya kutwaa Kombe la FA mwaka 2021, klabu ilishindwa kufanya "upasuaji" wa lazima kwenye kikosi. Walibaki na wachezaji wenye mishahara mikubwa huku ufanisi wao uwanjani ukianza kufifia.
Madudu ya usajili na mtego wa PSR
Dirisha la usajili la kiangazi la mwaka 2021 linatajwa kuwa "kaburi" la kwanza la Leicester. Klabu ilitumia mamilioni ya pauni kuwanunua wachezaji wenye majina makubwa kama kina Patson Daka, Boubakary Soumare, na Jannik Vestergaard. Tatizo halikuwa tu ununuzi huo, bali ni kushindwa kuwauza wachezaji nyota ili kusawazisha vitabu vya hesabu.
Hali hii ilipelekea klabu kukiuka sheria za faida na uendelevu (Profit and Sustainability Rules - PSR). Wakati viongozi waandamizi kama Wes Morgan na Kasper Schmeichel wakiondoka, pengo la uongozi uwanjani lilikuwa wazi. Matokeo yake yalikuwa ni klabu kushuka daraja hadi Championship mwaka 2023, tukio ambalo lilipaswa kuwa somo, lakini likageuka kuwa mwanzo wa makosa mapya.
Matumaini feki na kujirudia kwa historia
Baada ya kurejea Premier League kwa msimu mmoja chini ya Enzo Maresca, kulikuwa na mwanga wa matumaini. Lakini bodi ya Leicester ilifanya kosa lile lile la kutumia fedha ambazo hawakuwa nazo.
Waliwasajili Harry Winks na Conor Coady kwa mikataba ya gharama kubwa, jambo lililoivuta klabu tena kwenye rada za adhabu za EFL.
Uteuzi wa makocha uliofuata ulikosa dira. Steve Cooper hakuwahi kuungwa mkono na mashabiki kutokana na historia yake na mahasimu wao, Nottingham Forest. Baadaye, Ruud van Nistelrooy alikuja na rekodi mbaya, akipoteza michezo 18 kati ya 25. Hii ilionyesha wazi kuwa tatizo la Leicester lilikuwa kubwa kuliko mbinu za mwalimu, ulikuwa ni ugonjwa wa kimfumo uliokula mizizi ya klabu.
Uzembe wa uongozi: Boardroom failure
Moja ya shutuma nzito zinazoelekezwa kwa bodi ya Leicester ni ucheleweshaji wa maamuzi. Baada ya msimu wa maafa, klabu ilichukua wiki nne kumfuta kazi Van Nistelrooy, na wiki nyingine tatu kumpata Marti Cifuentes.
Ucheleweshaji huu uliharibu maandalizi ya msimu mpya na kuwavunja nguvu wachezaji.
Pigo lingine la kisaikolojia lilikuwa ni kuondoka kwa Jamie Vardy bila klabu kusajili mbadala wa hadhi yake. Vardy hakuwa tu mfungaji, bali alikuwa nembo ya Leicester. Bila yeye, timu ilipoteza utambulisho wake na uwezo wa kupambana (fighting spirit).
Anguko la mwisho na somo kwa dunia
Adhabu ya kukatwa alama sita kutokana na makosa ya kifedha ilikuwa "msumari wa mwisho kwenye jeneza." Licha ya Gary Rowett kupewa mikoba ya uokozi, jahazi lilikuwa limeshapata matundu mengi mno. Mechi dhidi ya Southampton, ambapo Leicester walipoteza uongozi wa 3-0 na kufungwa 4-3, ilidhihirisha kuwa morali ya timu ilikuwa imesambaratika kabisa.
Leo hii, uwanja wa King Power haushangilii tena ubingwa wa Premier League, bali unajiandaa kwa safari za mikoani huko League One dhidi ya timu ndogo. Hii ni taarifa ya onyo kwa klabu zote duniani, mafanikio ya uwanjani bila usimamizi madhubuti wa fedha na uongozi wenye maono ni kama nyumba iliyojengwa juu ya mchanga.
Leicester City imeporomoka, na safari ya kurejea juu itahitaji zaidi ya fedha, itahitaji mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi na kurejesha heshima ya klabu iliyowahi kuwa "kipenzi cha dunia." Kama alivyosema Jordan James, wengi walidhani haiwezekani, lakini sasa ni lazima wakubali ukweli na kuanza safari mpya kuanzia chini kabisa.
Leicester imetangazwa kushuka daraja ikiwa imecheza mechi 44 kati ya 46 inayotakiwa kucheza na kuvuna pointi 42, ikiwa nafasi ya 23 juu ya Sheffield inayoshika mkia.