Lautaro Martinez atengewa fungu Arsenal ikimtaka kikosini

Muktasari:
- Benchi la ufundi la Arsenal linataka kufanya maboresho kwenye kikosi chake kwa msimu ujao, na mmoja kati ya mastaa ambao limependekeza wasajiliwe ni Martinez mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Inter Milan kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu Italia (Serie A) kwa sasa.
ARSENAL imetakiwa kulipa Pauni 128 milioni katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa inaitaka saini ya mshambuliaji wa Inter Milan na timu ya taifa ya Argentina, Lautaro Martinez.
Benchi la ufundi la Arsenal linataka kufanya maboresho kwenye kikosi chake kwa msimu ujao, na mmoja kati ya mastaa ambao limependekeza wasajiliwe ni Martinez mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Inter Milan kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu Italia (Serie A) kwa sasa.
Mchezaji huyo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2029 katika msimu huu amecheza mechi 41 za michuano yote na kufunga mabao 19.
Mara kadhaa mabosi wa Barcelona pia wamekuwa wakionyesha nia ya kuitaka huduma ya nyota huyo, lakini wameshindwa kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kinachotakiwa na Inter Milan.
Jadon Sancho
CHELSEA iko tayari kuilipa Manchester United Pauni 5 milioni ili kuepuka kulipa Pauni 25 milioni zizonatakiwa kumsainisha mkataba wa kudumu winga huyo anayecheza kikosi hicho kwa mkopo. Sancho ambaye mkataba wake na Man United unamalizika 2026, wakati anatolewa kwa mkopo Chelsea kulikuwa na kipengele kinachoilazimisha kumchukua jumla.
Morgan Gibbs-White
KIUNGO wa Nottingham Forest na England, Morgan Gibbs-White, mwenye umri wa miaka 25, ni mmoja wa mastaa ambao Manchester City inataka kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kuziba pengo la kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Kevin de Bruyne, ambaye ataondoka mwisho wa msimu huu baada ya kudumu katika kikosi hicho kwa miaka 10.
Frank Onyeka
MABOSI wa Brentford wanataka kumrudisha kiungo wa kimataifa wa Nigeria, Frank Onyeka, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi licha ya kuwepo kwa timu mbalimbali zinazotaka kumsajili baada ya kiwango bora alichoonyesha katika kikosi cha Augsburg ambako anacheza kwa mkopo. Mkataba wake na Brentford unatarajiwa kumalizika 2027.
Christopher Nkunku
KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca anapanga kumuuza winga raia wa Ukraine, Mykhailo Mudryk, 24, na mshambuliaji kutoka Ufaransa Christopher Nkunku, 27, katika dirisha lijalo. Nkuku anadaiwa kuomba kuondoka kwa sababu haoni kama yupo katika mipango ya Enzo wakati Mudryk yupo kwenye uchunguzi juu ya matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni.
Merlin Rohl
MMABOSI wa Everton wanafanya mazungumzo na wawakilishi wa timu ya Freiburg wakijadili kumhusu kiungo wa timu hiyo, Merlin Rohl, 22, ambaye ni raia wa Ujerumani. Rohl ameonyesha kiwango bora tangu msimu uliopita wa michuano mbalimbali na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani. Katika msimu huu mchezaji huyo amecheza mechi 17 za michuano yote.
Joan Garcia
ARSENAL inapambana kulipa haraka Pauni 17 milioni kwa ajili ya kumsajili kipa wa Espanyol, Mhispania Joan Garcia ambaye mkataba wake unamalizika 2028. Mabosi wa Arsenal wanataka kufanikisha dili hilo haraka baada ya kuona kuna utitiri wa timu kibao kutoka Italia ambazo zimeanza kuiwania saini yake, hivyo inahofia kumkosa.
Arda Guler
ARSENAL inajiandaa kutoa ofa ya Euro 30 milioni kwenda Real Madrid ili kuipata saini ya kiungo Mturuki Arda Guler, 20, ambaye haridhishwi kutopewa nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza. Licha ya kutamani kuondoka, ripoti zinaeleza Madrid haina mpango wa kumwachia kwa sasa kwani inaamini atakuwa msaada siku za usoni.