Lampard apata ajira baada ya miezi 18
Muktasari:
- Lampard mwenye umri wa miaka 46 amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na timu hiyo ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Daraja la kwanza, England.
CONVERTY,ENGLAND: BAADA ya miezi 18 bila ya ajira hatimaye kocha wa zamani wa Chelsea, Everton na Derby County, Frank Lampard ametua baada ya kutangazwa kuwa kocha mpya wa Coventry City ya Championship.
Lampard mwenye umri wa miaka 46 amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na timu hiyo ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Daraja la kwanza, England.
Kocha hakuwa na timu tangu alipoachana na Chelsea mwisho wa msimu wa 2022/23 ambapo alipewa jukumu la kumalizia msimu baada ya kufukuzwa kwa Graham Potter.
Akizungumzia uteuzi wa Lampard, mmiliki wa Coventry, Doug King alisema: "Nashukuru kwamba Frank Lampard amekubali kujiunga na klabu yetu kama Kocha Mkuu. Frank aliwahi kufundisha timu kwenye ligi hii na anajua kinachohitajika katika ili kufanikiwa. Uzoefu wake pia akiwa na Chelsea na Everton pia utachangia sana kuleta maendeleo na fikra mpya katika timu yetu ili tufanikiwe."
Lampard anaingia katika kikosi hiki baada ya kutimuliwa kwa Mark Robins mapema mwezi huu na atasaidiana na makocha wengine wasaidizi Joe Edwards na Chris Jones, ambao amewahi kufanya kazi nao kabla.
Kwa mara ya kwanza kocha huyu alianza kufundisha Derby County mwaka 2018 ambayo aliisaidia kucheza mechi ya mtoano kuwania kupanda Ligi Kuu, baada ya hapo alitua Chelsea katika nyakati tofauti tofauti na pia aliwahi kufundisha Everton ambako kote hakufanya vizuri.