Lampard amuonya Pochettino

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa mpito wa Chelsea, Frank Lampard amemuonya Mauricio pochettino kwamba haitakuwa kazi rahisi kupindua meza baada ya kuteuliwa rasmi.

Vile vile Lampard akaiponda kiwango cha Chelsea baada ya kumaliza ligi nafasi ya 12 kwenye msimamo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1995-1996.

The Blues ilimaliza katika nafasi hiyo kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Newcastle United, mara ya mwisho iliweka rekodi mbovu zaidi ulikuwa msimu wa 1993-1994 kwani ilimaliza nafasi ya 14.

Lampard, ambaye alirejea Chelsea kama kocha wa mpito baada ya Graham Potter kufukuzwa kazi tangu Aprili, alikichambua kikosi kizima akidai kazi kubwa inahitajika.

"Ubora wa Chelsea umeporomoka kwa kiasi kikubwa, naongea ukweli kabisa, naweza nisionane na baadhi ya wachezaji baada ya hapa kwasababu nyingi tu," alisema Lampard

"Chelsea haikuwa na ushindani kabisa, haikucheza soka la kiwango cha juu, nilipokuja hapa nilitambua tu mambo sio shwari, bila shaka hata kocha mzuri akitokea anaweza kusaidia lakini wachezaji pia wanatakia kuwajibika asilimia 100, benchi la ufundi na mabosi kwa ujumla"

Baada ya Pochettino kusaini mkataba mpya kufuatia mazungumzo yaliodumu kwa muda wa wiki kadhaa, Lampard akamuonya kazi itakuwa ngumu kwasasabu mambo ya kubadilisha katika timu yatakuwa makubwa.

"Mimi ni nishabiki wa Pochettino, nadhani ni kocha mzuri, historia yake inakuonyesha alifundisha timu zenye viwango vikubwa, kwanza anatengeneza umoja ambao unaitambulisha timu ili ishinde kila mechi, lakini itachukua muda mrefu hadi kufikia huku, kazi ya kufanya ni kubwa kwahiyo haitakuwa rahisi," aliongeza

Pochettino hatakuwa na presha zaidi kwasababu Chelsea haitashiriki michuano ya Ulaya baada ya kuboronga kwahiyo atakuwa na muda wa kukijenga kikosi chake.

Licha ya kufanya usajili wa nguvu uliyogharimu Pauni 600 milioni ndani ya vipindi viwili vya usajili, Chelsea imefanya vibaya msimu huu, na ikatolewa katika mashindano ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, na ikakosa makombe yote ya ndani ya ligi.