Kwa nini Europa League muhimu Man United, Spurs

Muktasari:
Klabu hizo mbili, kila moja inahitaji ushindi kwenye mechi mbili tu zilizopo mbele yao ili kunyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kupitia mlango wa nyuma wa kubeba taji la Europa League.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United na Tottenham Hotspur zimeamua kuweka kando vita ya mapambano kwenye Ligi Kuu England na kuhamishia nguvu kwenye mchakamchaka wa kulisaka taji la Europa League.
Klabu hizo mbili kila moja inahitaji ushindi kwenye mechi mbili zilizopo mbele ili kunyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kupitia mlango wa nyuma wa kubeba taji la Europa League.
Man United na Tottenham kila moja imeshinda mechi yake ya kwanza ya hatua ya nusu fainali, ambapo moja ilishinda 3-0 ugenini wakati nyingine ilishinda 3-1 ikiwa nyumbani. Man United ilikuwa ugenini kucheza na Athletic Bilbao na Spurs ilikuwa nyumbani kukipiga na Bodoe/Glimt. Mechi za marudiano zitapigwa Alhamisi hii.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu England kama itashikilia uongozi wao wa mechi za kwanza, basi zitakwenda kukwaana kwenye mchezo wa fainali utakaofanyika huko Bilbao, Hispania.
Kushinda ubingwa wa Europa League, timu bingwa itapata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku Man United ikijiweka kwenye nafasi ya kuweka kibindoni mkwanja wa Pauni 85.8 milioni.
Kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa tiketi ya nafasi kwenye msimamo wa ligi ya ndani haiwezekani kwa timu hizo mbili, ambapo Man United inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo, moja juu ya Spurs, iliyopo kwenye nafasi ya 16.
Kutokana na hilo timu hizo mbili zimewekeza nguvu kubeba ubingwa wa Europa League, baada ya kuishuhudia Man United ikichapwa kwenye mechi nne na kutoka sare moja kati ya tano zilizopita ilizocheza kwenye Ligi Kuu England.
Kitu kama hicho kilitokea pia kwa Spurs, ambayo haijapata ushindi wowote tangu mwishoni mwa Februari ilipokipiga na Southampton.
Wakati huo, vita ya kushinda tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ligi ya ndani ni kali kutokana na timu kupigana vikumbo kuwania fursa hiyo ya kucheza michuano mikubwa ya Ulaya msimu ujao.
Hata hivyo, kushinda ubingwa wa Europa League ina maana inaweza kutoka nafasi kwa moja ya timu kati ya Man United au Spurs kunyakua tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao endapo kama zitafanikiwa kufika fainali ya Europa msimu huu.
Kama ni hivyo, je ni timu ngapi za Ligi Kuu England zitafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao?
Ushindi wa Arsenal dhidi ya Real Madrid hiyo ilihakikishia Ligi Kuu England kutoa timu tano kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa kutumia ligi ya ndani, kwa timu zilizoshika nafasi tano za juu kwenye msimamo.
Hiyo ina maana, Ligi Kuu England itakuwa na timu sita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao endapo kama Man United au Spurs itashinda ubingwa wa Europa League msimu huu.
Hiyo ni kwa sababu Man United na Spurs zitamaliza ligi nje ya tano bora, kutokana na tiketi moja ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kutengwa kwa ajili ya bingwa wa michuano namba mbili ya UEFA ukiweka kando zile tiketi za kufuzu michuano hiyo ya Ulaya kwa kupitia ligi za ndani.
Jambo hilo linazipa nafasi ya Manchester City, Newcastle United, Chelsea na Nottingham Forest kupambania tiketi hizo za kucheza michuano ya Ulaya baada ya Liverpool na Arsenal kujiweka kwenye uhakika mkubwa wa kuwamo kwenye michuano hiyo msimu ujao.
Kwa sasa, Liverpool ndiyo timu pekee iliyofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England. Newcastle kwa kushinda ubingwa wa Kombe la Ligi hilo linawapa nafasi ya kucheza Conference League kwa msimu wa 2025/26, endapo kama itashindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kupitia nafasi yao kwenye msimamo wa ligi.
Kama Newcastle itafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League kwa kupitia nafasi yao kwenye msimamo wa ligi, hivyo tiketi yao ya kucheza Conference League itahamia kwa timu itakayoshika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi na haijafuzu michuano ya Ulaya.
Kitu kama hicho kitatumika pia kwa bingwa wa Kombe la FA, ambaye anapaswa kucheza Europa League, tiketi yake itahamia kwa timu inayoshika nafasi ya juu kama wenyewe watafuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kushinda nafasi tano za juu kwenye msimamo.
Fainali ya Europa League, itapigwa Jumatano, Mei 21 kwenye Uwanja wa San Mames, Bilbao huko Hispania, uwanja wa Athletic Bilbao, ambao Man United ilitikisa nyavu mara tatu Alhamisi iliyopita ilipocheza na wenyeji hao.