Kwa Cavani mbona freshi tu

Saturday May 01 2021
CAVAN PIC

LONDON, ENGLAND. MSHAMBULIAJI wa Kimataifa  wa Uruguay, Edinson Cavani ametajwa kuwa yupo mbioni kukubali ofa aliyopewa na vigogo wa Manchester United  ya kuongeza mkataba wa mwaka mwingine mmoja wa kuendelea kuitumikia miamba hiyo ya soka la England.

Cavani,34, alijiunga na Manchester United, Oktoba mwaka jana akitokea Paris St-Germain kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza miezi mingine 12.

Inasemekana kwamba mshambuliaji huyo alikuwa na mpango wa kuondoka, lakini kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer alivunja  ukimya alhamisi  kwa kusema anahitaji kumwona akisalia kwenye kikosi chake.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha BBC huko nchini England, imefichuka kwamba  Solskjaer amechangia kwa kiasi kikubwa kwa Cavani kubadili maamuzi yake na yupo tayari kwa sasa kuendelea kusalia  Old Trafford.

Miongoni mwa mambo ambayo yanatajwa kumtibua Cavani na kutamani kuondoka England ni baada ya kipindi fulani kufungiwa kwa kile kinachosemekana kwamba alijihusisha na ubaguzi kupitia mitandao ya kijamii.

Licha ya kutoa ufafanuzi kwamba hakuwa na maana ovu chama cha soka England kilimweka hatiani na kumbidi Mruguay huyo kukosa michezo kadhaa huku akilipa pia faini kutokana na kosa hilo  la kibaguzi.

Advertisement

Kulikuwa na tetesi kwamba  Boca Juniors ya Argentina ilikuwa na mpango wa kumrejesha nyumbani, America ya Kusini mshambuliaji huyo ambaye alitupia mawili kwenye mchezo uliopita wa nusu fainali ya  Europa Ligi na kutoa asisti  tatu  wakati Manchester United ikiibuka na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya AS Roma.

Advertisement