Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutoka kiwandani hadi Kombe la Dunia, hadithi ya miujiza ya Deniz Undav

Muktasari:

  • Leo hii ndiye shujaa mpya wa Ujerumani katika Kombe la Dunia 2026.

HOUSTON, MAREKANI: MIAKA michache iliyopita, nyota wa timu ya taifa la Ujerumani,  Deniz Undav alikuwa akiamka saa 10 alfajiri kwenda kufanya kazi kiwandani ili kupafa fedha za  kujikimu na  maisha kabla ya kwenda mazoezini.

Leo hii ndiye shujaa mpya wa Ujerumani katika Kombe la Dunia 2026.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ameendelea kuandika historia yake baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiwezesha Ujerumani kutoka nyuma na kuifunga Ivory Coast mabao 2-1, ushindi uliowapeleka Wajerumani hatua ya 32 bora kwa mara ya kwanza tangu walipotwaa ubingwa wa dunia mwaka 2014.

Katika mashindano haya, Undav amekuwa silaha ya siri ya kocha Julian Nagelsmann. Akiwa amecheza mechi mbili akitokea benchi, tayari amehusika katika mabao matano, akifunga matatu na kutoa pasi mbili za mabao.

Takwimu hizo zimemfanya kufikia rekodi ya mkongwe wa Cameroon, Roger Milla, ambaye mwaka 1990 alihusika katika mabao matano akiwa mchezaji wa akiba.

Kilichofanya mafanikio hayo yawe ya kushangaza zaidi ni kwamba miezi michache iliyopita nafasi yake katika kikosi cha Kombe la Dunia ilikuwa mashakani.


ALIGOMBANA NA KOCHA WAKE

Mwezi Machi mwaka huu, Undav alijikuta kwenye mvutano wa wazi na kocha Julian Nagelsmann baada ya kufunga bao la ushindi dakika za mwisho dhidi ya Ghana.

Baada ya mchezo huo, mshambuliaji huyo alizungumza hadharani kuhusu ndoto yake ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Ujerumani.


Kauli hiyo haikumpendeza Nagelsmann. Kocha huyo alimjibu hadharani akisema Undav alikuwa anajiwekea presha isiyokuwa ya lazima na hata kudai kuwa huenda asingefunga bao hilo kama angeanza katika kikosi cha kwanza.

Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa nchini Ujerumani kabla ya Nagelsmann kuja baadaye kukiri kuwa alimwomba radhi mchezaji huyo.

Badala ya kujibizana, Undav aliamua kujibu kwa miguu yake uwanjani na tangu wakati huo amekuwa akionyesha kiwango bora kuliko wakati wowote katika maisha yake ya soka.


ALIKATALIWA KWA KUWA MFUPI

Safari ya Undav kuelekea Kombe la Dunia haikuwa rahisi. Akiwa na umri wa miaka 14, alikataliwa na akademi ya Werder Bremen baada ya kuambiwa hana mustakabali katika soka kutokana na kuwa na mwili mdogo.

Kauli hiyo ilimuumiza sana. "Nilivunjika moyo sana waliponiambia sina nafasi ya kufanikiwa kwa sababu nilikuwa mdogo kimwili," aliwahi kusema Undav.

Lakini hakukata tamaa. Akiwa na miaka 17 aliacha nyumbani kwa familia yake na kujiunga na klabu ya Havelse iliyokuwa ikicheza daraja la nne nchini Ujerumani.

Hapo ndipo maisha magumu yalianza.


MAISHA YA KIWANDANI

Wakati akicheza soka katika ligi ya daraja la nne, Undav alikuwa analipwa kiasi kidogo sana ambacho hakikutosha kuendesha maisha yake.

Kutokana na hali hiyo alilazimika kufanya kazi kiwandani kwa saa nane kila siku.

Kazi yake ilikuwa kuendesha mashine  katika kiwanda kimoja nchini Ujerumani.

Aliamka alfajiri kuelekea kazini, kisha moja kwa moja mazoezini kabla ya kurejea nyumbani usiku.

"Nilikuwa naamka saa 10 alfajiri, kwenda kiwandani, baada ya hapo mazoezini na kufika nyumbani karibu saa mbili usiku," anasema.

"Nilifanya kazi hiyo kwa sababu nilihitaji pesa za kuishi. Sikuweza kuishi kwa mshahara wa soka pekee."


UBELGIJI  ILIFUNGUA MILANGO

Baada ya miaka kadhaa ya kupambana, mwaka 2020 alijiunga na klabu ya Union Saint-Gilloise ya Ubelgji.

Huko ndipo maisha yake yalibadilika, aliisaidia timu hiyo kupanda daraja kabla ya kufunga mabao 25 katika ligi kuu ya Ubelgiji.

Ubora huo uliivutiab Brighton ya England iliyomsajili mwaka 2022 hata hivyo, maisha ya England hayakuwa rahisi.

Alifunga mabao matano pekee katika mechi 22 za Ligi Kuu England na baadaye akapelekwa kwa mkopo Stuttgart ya Ujerumani.

Wengi walidhani safari yake ya kucheza soka la kulipwa katika ngazi ya juu  imefikia mwisho lakini lakini ilikuwa mwanzo wa mafanikio makubwa zaidi.


STUTTGART ILIMFUFUA

Baada ya kuhamia Stuttgart moja kwa moja mwaka 2024, Undav alianza kuonyesha uwezo wake halisi.

Msimu uliopita wa Bundesliga alifunga mabao 19 na kumaliza nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora nyuma ya Harry Kane.

Mabao hayo ndiyo yaliyompa tiketi ya kwenda Kombe la Dunia.Na sasa analipa imani hiyo kwa kiwango kikubwa.

HAVERTZ HATARINI

Katika michezo miwili ya kwanza ya Kombe la Dunia, Nagelsmann amekuwa akimpa nafasi Kai Havertz kuanza.

Lakini kiwango cha Undav kinazidi kuweka presha kubwa. Kila anapoingia kutoka benchi anabadilisha mchezo.

Dhidi ya Curacao alifunga dhidi ya Ivory Coast amefunga tena mabao mawili.

Na sasa mjadala mkubwa nchini Ujerumani ni kama muda umefika kwa Nagelsmann kumpa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza dhidi ya Ecuador.

Kocha huyo mwenyewe amekiri kuwa anafikiria kufanya hivyo. "Ninaweza kumuanzisha. Kwa nini nivunje mfululizo wake mzuri?" anasema Nagelsmann.


NDOTO YA UBINGWA

Kwa sasa Undav amefunga mabao tisa katika mechi 11 za timu ya taifa ya Ujerumani. Ni takwimu zinazomuweka katika kundi la washambuliaji hatari zaidi duniani kwa sasa.

Kutoka kijana aliyekataliwa na Werder Bremen, mfanyakazi wa kiwandani aliyekuwa akipata mshahara mdogo hadi kuwa shujaa wa Kombe la Dunia.

Hiyo ndiyo hadithi ya Deniz Undav.

Na kama ataendelea na kiwango hiki, huenda safari yake ya miujiza ikaishia mikononi akiwa amebeba kombe kubwa zaidi katika soka la dunia huku Ujerumani ikisaka taji lake la tano la Kombe la Dunia.