Kutoka dakika 30 bila kugusa mpira hadi kwenye historia Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika mechi ya kwanza ya ufunguzi kati ya Hispania na Cape Verde iliyoisha suluhu ya (0-0), Juni 15, 2026, nyota huyo aliandika rekodi ya kucheza dakika 30 za kwanza bila ya kugusa mpira ikiwa ni historia ya Kombe la Dunia la FIFA tangu mara ya mwisho ilipotokea hivyo mwaka 1966.
ATLANTA, MAREKANI: BAADA ya mshambuliaji wa Hispania, Mikel Oyarzabal kuandika rekodi mbovu ya kucheza dakika 30 bila ya kugusa mpira katika mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Cape Verde, nyota huyo ameandika historia nyingine japo safari hii ni ya kuvutia.
Katika mechi ya kwanza ya ufunguzi kati ya Hispania na Cape Verde iliyoisha suluhu ya (0-0), Juni 15, 2026, nyota huyo aliandika rekodi ya kucheza dakika 30 za kwanza bila ya kugusa mpira ikiwa ni historia ya Kombe la Dunia la FIFA tangu mara ya mwisho ilipotokea hivyo mwaka 1966.
Baada hapo, hatimaye leo nyota huyo ameandika rekodi mpya akiwa ni mchezaji wa tatu kuhusika na mabao matatu iwe kwa kufunga au kutoa asisti katika Kombe la Dunia tangu mara ya mwisho ilipotokea mwaka 1966.
Mshambuliaji huyo wa Klabu ya Real Sociedad ya Hispania, ameandika rekodi hiyo baada ya kuhusika na mabao matatu ya dakika 24 za kipindi cha kwanza, kufuatia kufunga mawili na kutoa asisti moja kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 4-0 dhidi ya Saudi Arabia.
Nyota huyo aliasisti bao la kwanza la Hispania lililofungwa na Lamine Yamal dakika ya 10, kisha yeye kufunga mawili dakika ya 21 na 24, kisha Hassan Al-Tambakti akajifunga na Saudi Arabia kuchapwa mabao 4-0 katika mechi ya pili ya kundi H.
Rekodi hiyo ya kuhusika katika mabao matatu ya Kombe la Dunia kwa dakika 30, za kwanza ilikuwa inashikiliwa na wachezaji wawili walioiweka katika fainali za Kombe la Dunia lililofanyika mwaka 1966 nchini England.
Nyota wa kwanza kuandika rekodi ya kufunga au kutoa asisti ya bao ndani ya dakika 30, alikuwa ni Eusebio wa Ureno aliyefunga mabao manne katika hatua ya robo fainali na timu hiyo kushinda 5-3 dhidi ya Korea Kaskazini, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Goodison Park, Julai 23, 1966.
Mchezaji wa pili kuweka rekodi hiyo ni Geoff Hurst wa England aliyefunga mabao matatu (Hat-Trick), katika mechi ya fainali ya ushindi wa kikosi hicho wa mabao 4-2 dhidi ya Ujerumani Magharibi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Julai 30, 1966, kwenye Uwanja wa Wembley, ndio inayobaki katika kumbumbuku za mashabiki wa England kwani ndio taji pekee la Kombe la Dunia iliyowahi kuchukua, huku ikiwa ndio mwenyeji.