Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kundi C Kombe la Dunia laanza kuchora picha ya mtoano

Muktasari:

  • Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kudhani Brazil na Morocco tayari wameweka mguu mmoja hatua ya 32 Bora lakini ukiangalia kwa undani zaidi utaona bado hakuna timu iliyojihakikishia nafasi hiyo.

PHILADELPHIA, MAREKANI: KATIKA makundi yote 12 ya Kombe la Dunia 2026, huenda hakuna kundi ambalo limeanza kuvutia kama Kundi C baada ya mechi mbili kwa kila timu, Brazil na Morocco  zikiwa na pointi nne kila moja, Scotland ikiwa na pointi tatu huku Haiti ikibaki bila pointi.

Kwa mtazamo wa kawaida unaweza kudhani Brazil na Morocco tayari wameweka mguu mmoja hatua ya 32 Bora lakini ukiangalia kwa undani zaidi utaona bado hakuna timu iliyojihakikishia nafasi hiyo.

Hili ndilo kundi ambalo limebeba simulizi nyingi kwa wakati mmoja. Kuna Brazil inayojaribu kurejesha heshima yake ya kuwa miongoni mwa vigogo wa dunia, Morocco inayotaka kuthibitisha kuwa mafanikio yake ya miaka ya karibuni hayakuwa bahati, Scotland inayopambana kurejea kwenye ramani ya soka la dunia na Haiti ambayo licha ya kupoteza mechi mbili bado inaweza kuathiri hatima ya wengine.

Kilichofanya kundi hili liwe la kuvutia zaidi ni kwamba baada ya mechi mbili hakuna timu iliyoonyesha ubabe wa kutisha dhidi ya wapinzani wote.

Brazil ilianza kwa sare ya bao 1-1  dhidi ya Morocco kabla ya kuifunga Haiti mabao 3-0. Morocco ikatoa sare na Brazil kisha kuifunga Scotland 1-0.

Scotland ikaifunga Haiti 1-0 lakini ikashindwa dhidi ya Morocco. Hiyo inaonyesha tofauti ya viwango si kubwa kama ambavyo wengi walidhani kabla ya mashindano.


MOROCCO IMEBADILI SIMULIZI

Kama kuna timu ambayo imeonyesha kuwa na kitu kikubwa  cha kuonyesha katika kundi hili basi ni Morocco.

Baada ya kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu kama mafanikio hayo yangekuwa mwanzo wa zama mpya.

Kilichoonekana kwenye mechi mbili za kwanza kinaonyesha Wamorocco bado wanaendelea kukua.

Sare dhidi ya Brazil iliwapa kujiamini. Ushindi dhidi ya Scotland umeonyesha wanaweza kushinda hata pale wanapopewa jukumu la kutawala mchezo.

Tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ambapo timu nyingi za Afrika zilijulikana zaidi kwa nguvu na kasi, Morocco sasa inaonyesha utulivu wa kiufundi, uwezo wa kumiliki mpira na nidhamu ya kimfumo.

Ndiyo maana mechi yao ya mwisho dhidi ya Haiti ni muhimu sana. Ushindi utaifanya ifike pointi saba ambazo mara nyingi zinatosha kumaliza juu au katika nafasi mbili za kwanza za kundi.


BRAZIL BADO NI BRAZIL, LAKINI...

Brazil inaongoza kundi kwa tofauti ya mabao, lakini ukweli ni kwamba bado haijatoa ujumbe wa kutisha kwa washindani wake.

Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Haiti ulionyesha ubora wa kikosi chao, lakini kipimo halisi kilikuwa dhidi ya Morocco ambapo walionekana kupata wakati mgumu.

Kitu kinachoweza kuwapa wasiwasi mashabiki wa Brazil ni kwamba katika michuano ya kisasa timu zinazofika mbali si lazima zile zenye vipaji vingi zaidi, bali zile zenye mfumo bora zaidi. Hadi sasa Morocco imeonekana kuwa na mfumo ulio imara kuliko Brazil.

Ndiyo maana mchezo wa mwisho dhidi ya Scotland unaweza kuwa mtihani mkubwa kuliko wengi wanavyofikiri. Scotland inaingia uwanjani ikijua ushindi unaweza kuibeba moja kwa moja kwenda hatua inayofuata.


SCOTLAND BADO INA NAFASI

Kama kuna timu ambayo inaweza kuharibu hesabu zote za kundi hili basi ni Scotland.

Ina pointi tatu tayari. Hiyo ina maana ushindi dhidi ya Brazil utaifikisha pointi sita na kuifanya iwe katika nafasi nzuri sana ya kufuzu.

Hata sare inaweza kuipa matumaini makubwa kutegemea matokeo ya Morocco dhidi ya Haiti na hesabu za timu bora ambazo zitashika nafasi ya tatu.

Tatizo kubwa kwa Scotland ni kwamba inakutana na timu yenye uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa. Brazil imecheza mechi za presha kama hizi mara nyingi zaidi kuliko karibu timu yoyote duniani.

Lakini presha pia inaweza kuwa upande wa Brazil. Wabrazil wanajua kushindwa kunaweza kuwafanya washuke hadi nafasi ya tatu au hata kuhatarisha nafasi yao ya kufuzu.


HAITI INAWEZA KUWA MWAMUZI

Mara nyingi timu zinazopoteza mechi mbili za kwanza huonekana kama wasindikizaji tu wa mashindano. Lakini Haiti inaweza kuwa na neno la mwisho katika kundi hili.

Ikiifunga Morocco, hesabu zote zitabadilika ghafla.

Ingawa hilo linaonekana gumu kutokana na kiwango walichoonyesha hadi sasa, historia ya Kombe la Dunia imejaa matokeo yaliyowashangaza wengi.

Mara nyingi timu ambazo tayari zimeonekana kuwa nje ya mashindano huingia uwanjani bila presha yoyote na kuwa hatari zaidi.


KINACHOWEZA KUTOKEA SIKU YA MWISHO

Hali rahisi zaidi ni Brazil na Morocco kushinda mechi zao. Hapo zote zitafikisha pointi saba na kufuzu moja kwa moja.

Lakini kama Scotland itaifunga Brazil, kundi litakuwa na mwelekeo tofautu. Brazil inaweza kujikuta ikitegemea tofauti ya mabao. Morocco inaweza kuongoza kundi au kushuka nafasi ya pili kulingana na matokeo yake.

Kama Brazil na Scotland watatoa sare, Scotland itafikisha pointi nne na kuanza kuhesabu nafasi yake kama moja ya timu bora za nafasi ya tatu.

Ndiyo maana mechi za mwisho za kundi hili si mechi za kawaida. Ni dakika 90 ambazo zinaweza kubadilisha mwelekeo nzima ya kundi.


KUNDI LA WASHINDANI WATATU

Kwa sasa picha inayoonekana ni kwamba Haiti imebaki nyuma, lakini kati ya Brazil, Morocco na Scotland kila mmoja bado ana sababu ya kuamini.

Brazil ina historia na ubora wa kikosi.

Morocco ina mfumo na kujiamini.

Scotland ina matumaini na hamasa ya kushtukiza.

Ndiyo maana Kundi C limekuwa moja ya makundi yanayovutia zaidi katika Kombe la Dunia 2026 na kama mechi mbili za kwanza zimeonyesha chochote, ni kwamba hakuna anayepaswa kuamini kazi imekwisha kabla ya filimbi ya mwisho ya mechi za  Juni 24.