Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uholanzi na rekodi bora inayotesa kwa miaka 20

Muktasari:

  • Ushindi wa mabao 5-1 ilioupata Uholanzi leo Juni 20, 2026 dhidi ya Sweden katika mechi ya hatua ya makundi iliyopigwa kwenye Uwanja wa NRG, Houston nchini Marekani, umeifanya timu hiyo kuendelea kushikilia rekodi ambayo kwa sasa inakaribia miaka 20.

TIMU ya taifa ya Uholanzi imeendelea kushikilia rekodi ya kutopoteza mechi ya Kombe la Dunia ndani ya dakika 90, tangu mara ya mwisho kwa kikosi hicho maarufu kwa jina la 'Orange' kuchapwa mwaka 2006, katika fainali hizo zilizofanyika nchini Ujerumani.

Ushindi wa mabao 5-1 ilioupata Uholanzi leo Juni 20, 2026 dhidi ya Sweden katika mechi ya hatua ya makundi iliyopigwa kwenye Uwanja wa NRG, Houston nchini Marekani, umeifanya timu hiyo kuendelea kushikilia rekodi ambayo kwa sasa inakaribia miaka 20.

Mechi ya mwisho kwa timu ya taifa ya Uholanzi kupoteza ndani ya dakika 90, ilikuwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Ureno katika pambano la hatua ya 16, bora lililopigwa Juni 25, 2006, ambapo kuanzia hapo hadi leo inaendelea kushikilia rekodi yake.

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, zilizofanyika Afrika Kusini, Uholanzi ilicheza mechi saba, kati ya hizo ilishinda sita na sare moja ndani ya dakika 90, ambapo mechi ya sare ilikuwa 0-0 dhidi ya Hispania iliyokuwa ni ya fainali kwa kuchapwa bao 1-0, la dakika za nyongeza na sio zile 90.

Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, Uholanzi ilicheza mechi saba na kati ya hizo ilishinda tano na kutoka sare mbili kwa muda wa dakika 90, ambapo mwaka huo ilimaliza nafasi ya tatu baada ya kuwachapa wenyeji Brazil kwa mabao 3-0, Julai 12, 2014.

Timu hiyo haijashiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 huko Urusi, ila nchini mwaka 2022 Qatar ilishiriki na kucheza mechi tano za dakika 90 bila ya kupoteza, ambapo kati ya hizo ilishinda tatu na kutoka sare mbili ikiendeleza rekodi ya kuvutia kwa kikosi hicho cha Orange.

Katika fainali hizo za Qatar, Uholanzi iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa na Argentina kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lusail, Desemba 9, 2022.

Katika fainali za 2026, zinazofanyika nchi za Marekani, Mexico na Canada, Uholanzi iko kundi F ambapo ilianza kampeni za michuano hiyo kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Japan, kisha kuishushia mvua yamabao Sweden kwa kuichapa 5-1 na kujikita kileleni mwa kundi hilo lenye timu nyingine ya Tunisia inayowakilisha Bara la Afrika.

Licha ya rekodi hiyo bora ya kuvutia, ila Uholanzi haijawahi kushinda taji la Kombe la Dunia, mafanikio zaidi ni kumaliza nafasi ya pili mara tatu mwaka 1974, 1978 na 2010, huku nafasi ya tatu ikishika mara moja ambapo ni mwaka 2014, nchini Brazil.