Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KUNANI? Real Madrid ikizidi kuzama, Barcelona ikinusa ndoo LaLiga

Muktasari:

  • Katika mchezo huo, Real Madrid ilionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuondoka na pointi zote tatu baada ya Vini­cius Junior kufunga bao la kuongoza mapema. Hata hivyo, kushindwa kulinda bao hilo kuliigharimu ambapo Hector Bellerín alisawazisha katika dakika ya 94 na kuipa Betis sare muhimu.

MADRID, HISPANIA: MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) msimu huu huenda ziko hatua ya mwisho yenye presha kubwa, baada ya Real Madrid, juzi, Ijumaa kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Real Betis katika matokeo ambayo yamezidisha pengo na vinara Barcelona, jambo ambalo limebadilisha mwelekeo wa ligi hiyo.

Katika mchezo huo, Real Madrid ilionekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuondoka na pointi zote tatu baada ya Vini­cius Junior kufunga bao la kuongoza mapema. Hata hivyo, kushindwa kulinda bao hilo kuliigharimu ambapo Hector Bellerín alisawazisha katika dakika ya 94 na kuipa Betis sare muhimu.

Matokeo hayo yamewaweka Real Madrid katika nafasi ngumu ya ubingwa wakiwa nyuma kwa pointi nane dhidi ya Barcelona ambayo, jana, Jumamosi ilishuka dimbani kucheza dhidi ya Getafe.

Barcelona sasa wako katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa huo huku wakiwa na kibarua cha kufanya vizuri katika mechi tano zilizosalia, huku Real Madrid wakilazimika kushinda karibu kila mchezo uliosalia ili kusikilizia nini kitatokea kwa wapinzani wao.

Kwa Real Madrid, ratiba iliyosalia inaonyesha ugumu mkubwa. Wamebakiwa na mechi tano pekee ikiwa ni ugenini dhidi ya Espanyol kisha pambano la Dabi ya Hispania (El Clasico) dhidi ya Barcelona ugenini, mechi ya nyumbani dhidi ya Real Oviedo kisha safari ngumu ugenini dhidi ya Sevilla na kumalizia nyumbani dhidi ya Athletic Club.

Hii ina maana Madrid wana jumla ya pointi 15 pekee zinazoweza kupatikana na kwa hali ya sasa, hawana tena nafasi ya makosa yoyote ikiwa wanataka kuendelea kuweka presha kwa Barcelona.

Kwa upande wa Barcelona, kikosi cha Hansi Flick kina mechi tano, jambo linalowapa nafasi ya kuongeza tofauti ya pointi. Baada ya kumalizana jana dhidi ya Getafe, wataenda tena ugenini kucheza dhidi ya Osasuna, kabla ya mchezo muhimu sana wa El Clásico dhidi ya Real Madrid.

Baada ya hapo, Barcelona watakutana na Alaves ugenini, kisha Real Betis nyumbani na kumalizia msimu dhidi ya Valencia ugenini. Ratiba hii inaonekana kuwa na changamoto, lakini pia inawapa nafasi ya kudhibiti mbio za ubingwa.

El Clasico ya Mei 10 kati ya Barcelona na Real Madrid inabaki kuwa mchezo mkubwa zaidi wa msimu, lakini inaweza isiwe na uzito wa kuamua ubingwa kama Barcelona wataendelea kushinda mechi zao nyingine kabla ya hapo.

Madrid kwa upande wao wanakabiliwa na tatizo kubwa la kupoteza pointi katika mechi muhimu, hasa baada ya kushindwa kulinda uongozi dhidi ya Betis. Barcelona, licha ya kumpoteza Lamine Yamal kutokana na jeraha litakalomweka  nje ya uwanja kwa msimu mzima, bado wanaonekana kuwa na kikosi kipana na chenye ubora wa kutosha kuendelea kupambania ubingwa huo.

Kwa Madrid, tegemeo kubwa limebaki kwa Vini­cius Junior na Kylian Mbappe, lakini tatizo la kujilinda na kushindwa kumaliza mechi mapema linaendelea kuwa changamoto kubwa katika mbio hizi za ubingwa.

Real Madrid imeshinda mechi moja katika tano zilizopita katika mashindano yote, imeshinda dhidi ya Alaves kwa mabao 2-1, imetoa sare mbili dhidi ya Betis na Girona kwa bao 1-1 katika kila mchezo huku ikifungwa nyumbani (2-1) na ugenini (4-3) dhidi ya Bayern Munich katika ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa jumla, hali ya sasa inaonyesha Barcelona wakiwa karibu zaidi na taji la La Liga, huku Madrid wakihitaji muujiza wa kushinda kila mechi iliyosalia na kusubiri Barcelona wapoteze pointi nyingi.