Kuna timu hii ya bure kabisa
Muktasari:
- Liverpool imefanya matumizi kufikia Pauni 400 milioni endapo itavunja rekodi ya Uingereza kumnasa straika Alexander Isak.
LONDON, ENGLAND: WAKATI dirisha la usajili likielekea ukingoni, klabu za Ligi Kuu England hazina woga kufungua pochi ili kunasa mastaa wapya.
Liverpool imefanya matumizi kufikia Pauni 400 milioni endapo itavunja rekodi ya Uingereza kumnasa straika Alexander Isak.
Arsenal, Manchester City, Chelsea na Manchester United zimetumia pesa nyingi. Kwa hali ilivyo, kuna timu zitaendelea kusajili mastaa kabla ya dirisha halijafungwa Septemba Mosi.
Kuna wachezaji kibao wapo huru kama Christian Eriksen, Victor Lindelof, Jamie Vardy na Kurt Zouma ambao hawana timu. Lakini, fursa ya kunasa huduma za mastaa wenye vipaji vikubwa mwaka 2026 inaonekana kuwa tamu zaidi kutokana na kundi kubwa wanaomaliza mikataba msimu huu.
Kikosi cha kwanza kinachokaribia thamani ya Pauni 350 milioni kitapatikana bure ndani ya miezi 12 ijayo kwa mujibu wa Sportingpedia. Kwa kuzingatia hilo, hii hapa orodha ya mastaa ambao wanaweza kuunda kikosi kizima huku huduma zao zikipatikana bure kabisa nyakati kama hizi mwakani.
Golini kuna wachezaji wengi lakini kipa Mtaliano, Gianluigi Donnarumma linaweza kuwa chaguo bora kutokana na mkataba wake kubaki mwaka mmoja tu PSG na kama hatahama au kusaini dili jipya atakuwa huru dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kwenye safu ya ulinzi, kuna mkali wa Everton, Vitalii Mykolenko amebakiza mwaka mmoja na saini yake inaweza kugharimu Pauni 24 milioni. Staa wa Crystal Palace, Marc Guehi, naye amebakiza mwaka na Liverpool inamtaka kwa Pauni 38.8 milioni. Kikosi hicho pia kinaweza kuwa na huduma ya Ibrahima Konate, anayethaminishwa kwa Pauni 51 milioni na Dayot Upamecano Pauni 43 milioni. Beki wa Real Madrid, Raul Asencio ana-weza kucheza kulia thamani yake ni Pauni 34.5 milioni.
Kwenye kiungo kuna kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong alihusishwa mara nyingi na Manchester United akithaminishwa kwa Pauni 38.8 milioni, lakini anaweza kupatikana bure mwakani.
Sambamba na hilo kuna Rodrigo Bentancur na Bernardo Silva wanaweza kuondoka Tottenham na Man City mtawalia kweye dirisha lijalo ambapo thamani ya wote hao ni Pauni 58.7 milioni.
Na kwenye fowadi, straika wa Juventus, Dusan Vlahovic naye amebakiza mwaka kwenye mkataba wake na thamani yake ni Pauni 30.2 milioni, huku fowadi wa Brentford, Yoane Wissa, naye akiingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake na thamani yake ni Pauni 27.6 milioni.
Kikosi chenyewe cha bure 2026: Donnarumma; Asencio, Guehi, Konate, Upamecano, Mykolenko; De Jong, Silva, Bentancur; Wissa, Vlahovic.