Kuna shughuli nzito EPL, Man City yatajwa

Muktasari:
- Timu hizo ni zile zinazokamata nafasi ya tatu hadi ya saba na hapo zikiwa zimesalia mechi hizo saba lolote linaweza kutokea kwa miamba hiyo.
LONDON, ENGLAND: KATIKA kinyang’anyiro cha Ligi Kuu England, baada ya ishu ya ubingwa, kuna vita nyingine inaamuliwa. Nani atashinda, ndiyo hadi filimbi ya mwisho.
Liverpool tayari imeshaanza kunusa harufu ya kombe, haina wasiwasi pale juu ikiongoza msimamo kwa tofauti ya pointi 11 dhidi ya Arsenal na sasa vita inayoangaliwa ni ya nani na nani watazifuata miamba hiyo Ligi ya Mabingwa Ulaya na zenyewe tayari zina uhakika.
Timu hizo ni zile zinazokamata nafasi ya tatu hadi ya saba na hapo zikiwa zimesalia mechi hizo saba lolote linaweza kutokea kwa miamba hiyo.
Timu ya kwanza iliyo katika vita hiyo ni mabingwa watetezi Manchester City ambao wanashika nafasi ya sita katika msimamo wa pointi zao 52.
Kijumla imebakisha mechi saba na itacheza na Aston Villa inayoonekana kuwa bora kwa misimu miwili ya hivi karibuni pia itaumana na Fulham yenye rekodi nzuri mbele ya vigogo wa EPL ikiwa imetokea kushinda mabao 3-2 dhidi ya Liverpool wikiendi iliyopita.
Nafasi ya kufuzu bado ipo kwani, tofauti yake na Nottingham Forest inayoshika nafasi ya tatu ni pointi tano tu, ambazo inaweza kuzifikia kwa haraka ikiwa Forest itafanya vibaya katika michezo yake miwili kati ya saba iliyobaki.
Nottingham ni timu nyingine katika vita hii, ikiwa inashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 57. Licha ya kuonekana ina uwezekano mkubwa wa kutoboa na kufuzu, bado inaweza kujikuta nje ya nafasi tano za juu ikiwa itashindwa kuchanga karata zake vizuri katika michezo kadhaa iliyobakia.
Forest inakabiliwa na mechi mbili za vigogo kati ya saba zilizobakia na italazimika kwenda London kucheza dhidi ya Tottenham kisha itaikaribisha Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani wa City Ground ambao tangu kuanza kwa msimu huu imepoteza mechi mbili tu.
Mbali ya vigogo hao pia itakuwa na mechi dhidi ya Crystal Palace na West Ham, vilevile itakuwa na mechi tatu za nyumbani ambazo ni dhidi ya Everton, Brentford na Leicester City.
Aston Villa ambayo inaweza kufuzu pia ikiwa itashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako ipo hatua ya robo fainali jambo linaloonekana kuwa gumu, njia pekee inayoonekana huenda ikawa rahisi kwao ni kumaliza katika nafasi tano za ligi.
Kwa sasa vijana hawa wa Unai Emery wapo nafasi ya saba wakiwa na pointi 51 tofauti ya pointi sita kati yao na Forest inayoshika nafasi ya tatu.
Newcastle ambayo hadi sasa ina uhakika wa kucheza michuano ya Uefa Conference League baada ya kutwaa kombe la Carabao kwa kuichapa Liverpool mabao 2-1, pia ipo katika vita hii ya Uefa.
Kwa sasa timu hii inayomilikiwa na matajiri kutoka Saudi Arabia ipo nafasi ya tano ikiwa na alama 53, ambazo ni tofauti ya alama nne kati yao na timu inayoshikila nafasi ya tatu.
Nafasi hii iliyokuwepo ikiwa italamaliza inaweza kufuzu Ligi ya Mabingwa lakini bado hakuna uhakika kwani Aston Villa na Manchester City zote zinaweza kuishusha ikiwa itapoteza au kutoa sare katika mchezo mmoja tu.
Presha kubwa iliyopo kwa mashabiki wa timu hii ni aina ya mechi ambazo imebakisha kabla ya kumaliza msimu na itakutana na Arsenal, Manchester United na Chelsea ambazo zina ugumu kutokana na ukubwa wa timu.
Chelsea ambayo inashikilia nafasi ya nne kwa pointi 53, pia haiko salama na inaweza kujikuta nje ya orodha ya timu zilizofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya mwisho wa msimu huu.
Kwanza kabisa mechi saba zilizobaki, itaumana na Liverpool, Newcastle, Man United Nottingham Forest ambazo zote zinaonekana kuwa ngumu kwao kutoka na viwango vya timu hizo na wachezaji walionao.
Kuangusha alama hata moja kati mechi nne kati ya saba inaweza kuwa ndio mkono wa kwaheri kwao.