Kumekucha! macho yote Qatar

DOHA, QATAR. UFUNGUZI rasmi wa fainali za 22 Kombe la Dunia 2022 unafanyika leo nchini Qatar mwenyeji wa michuano hiyo huku kukiwa na mambo mengi yatakayofanyika kusherehesha michuano hiyo mikubwa.

Qatar inaandaa michuano hii ikiwa ni nchi ya 80 kushiriki kwani ndio inafuzu kwa mara ya kwanza tena kwa bahati ya kuwa mwenyeji.

Fainali hizi ambazo zilianza mwaka 1930 nchini Uruguay zinashirikisha mataifa 32 na mbali na mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Qatar dhidi ya Ecuador, kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali duniani.

Hata hivyo, kumekuwa na mambo mengi kabla ya ufunguzi huo ikiwamo Qatar kushutumiwa kutoa hongo kwa wapinzani wao Ecuador ili iwaachie ushindi kwenye mchezo huo.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka duniani bado halijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo na jana Rais wake, Gianni Infantino alifanya mkutano na wanahabari kuhusu ufunguzi wa michuano hiyo.


UWANJA UTAKAOTUMIKA

MAHALI: Al Kohr, Qatar

UWANJA: Al Bayt Stadium

MUDA: Saa 1:00 usiku


KIKOSI KINACHOWEZA KUANZA

Qatar huenda ikatumia mfumo wa 3-5-2 dhidi ya Ecuador kwenye mchezo huo ambao nyota wanaotazamiwa kuanza ni Sheeb, Khoukhi, Rawi, A Hassan; Ro-Ro, Hatem, Haydos, Boudiaf, Amin; Afif na Ali. Wachezaji wa akiba: Y Hassan, Barsham, Waad, Salman, Kheder, Mohammad, Assadalla, Hajri, Madibo, Hadhrami, Gaber, Meshaal, Alaaeldin, Muntari na Muneer. Qatar itakuwa chini ya Kocha Felix Sanchez.


TAARIFA KIKOSI CHA QATAR

Qatar ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Albani, nyota wa timu hiyo Akram Afif akianzia benchi, Afif alicheza sambamba na Almoe Ali ambaye alifunga bao pekee katika mtanange huo.

Afif ndiye mchezaji anayekubalika sana na mashabiki Qatar na licha ya kutopewa nafasi kubwa imepania kupeperusha bendera ya nchi hiyo katika mechi yao ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia ambazo zinafanyika kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.


KIKOSI CHA ECUADOR

Mfumo utakaotumika ni 4-2-3-1

Wachezaji wanaoweza kuanza ni Dominguez, Arboleda, Torres, Hincapie, Estupinan; Mendez, Caicedo; Plata, Cifuentes, Ibarra na Valencia. Wachezaji wa akiba: Galindez, Ramirez, Pacho, Arreaga, An Preciado, Palacios, Porozo, Gruezo, Ay Preciado, Mena, Sarmiento, Franco, Estrada, Reasco na Rodriguez.


WASANII WATAKAOTUMBUIZA

Wasanii wataombuiza katika hafla ya ufunguzi wa michuano hii ni rapa maarufu kutoka Marekani, Lil Babay, Davido, Ozuna, Gims, Trinidad Cardona. Wasanii hawa wataimba nyimbo maalumu za fainali za Kombe la Dunia.


MASHABIKI

Mashabiki wa soka wapo tayari kwaajili ya mechi hiyo ya ugunguzi ambayo itachezwa katika uwanja wa Al Bayt.

Uwanja huu unaingiza jumla ya mashabiki 60000, imeelezwa mashabiki walianza kukata tiketi mapema ili kuepukana na usumbufu wowote utakaojitokea.


HALI YA HEWA

Mashabiki na wachezaji watakumbana na hali ya joto na upepo kwani ndio kipindi chake kwasasa Qatar. Aidha viwanja vyote vitakavyotumika mechi za Kombe la Dunia zimewekewa kifaa maalumu cha kupunguza joto hivyo mashabiki hawatapata tabu wakati wanaanglia mechi. Hali ya hewa ya joto ya Qatar nbi nyuzi 29 na huenda ikapanda hadi nyuzi 30.