Kumekucha Arsenal, Arteta kushusha vyuma Januari
Muktasari:
- Wakati miamba hiyo ya Emirates ikichuana kwenye anga za juu za Ligi Kuu England, kocha Arteta anaamini bado kuna maeneo yenye uzoefu kwenye kikosi chake na hivyo anahitaji marekebisho na maboresho.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri kwamba atafanya jambo kwenye dirisha la usajili la Januari ili kukiongezea nguvu kikosi chake.
Wakati miamba hiyo ya Emirates ikichuana kwenye anga za juu za Ligi Kuu England, kocha Arteta anaamini bado kuna maeneo yenye uzoefu kwenye kikosi chake na hivyo anahitaji marekebisho na maboresho.
Katika kuelekea mechi ya Aston Villa, Arteta amesema: “Sijui hakika itakuwaje, lakini tunatambua kinachotukabili, pale kwenye eneo la ushambuliaji na kwenye beki, tunachohitaji ni kuwa na kikosi kipata kama ilivyo kwa timu nyingine, zina wachezaji 24 hadi 25.
“Ndiyo hivyo. Sawa tuna majeruhi wengi kuliko tulivyotarajia, lakini kuna maeneo hayazuiliki, tunataka kitu muhimu kwenye timu ili kuwa na wachezaji watakaokuwa wanacheza msimu huu.
“Inategemea, kama nilivyosema tutaangalia wachezaji waliopo, hivyo, dirisha likifunguliwa, sisi Arsenal tutakwenda kutazama tunahitaji nini? Na tutakapoona tutafahamu sasa, tusajili au tuache, lakini kazi yetu kila siku vitu vinatokea.”
Arsenal ilikabiliwa na mechi muhimu dhidi ya Aston Villa katika vita ya kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, ikijaribu kusaka taji hilo baada ya kukaribia kulinyakua kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo, wakati ilipomaliza nafasi ya pili, mara mbili nyuma ya Manchester City na moja nyuma ya Liverpool.