Kumbe Onana alitaka aongezwe mshahara
Muktasari:
- Onana, 29, ambaye alifanya ovyo kwenye goli msimu uliopita alipofanya makosa kadhaa yaliyogharimu timu yake, aliwasiliana maombi ya kupewa dili mpya na lenye maboresho, wakati kiwango chake kilikuwa moja ya sababu ya timu hiyo kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amekasirishwa na Andre Onana baada ya kuwasilisha maombi ya kutaka mkataba mpya wakati aliporejea kwenye pre-season.
Onana, 29, ambaye alifanya ovyo kwenye goli msimu uliopita alipofanya makosa kadhaa yaliyogharimu timu yake, aliwasiliana maombi ya kupewa dili mpya na lenye maboresho, wakati kiwango chake kilikuwa moja ya sababu ya timu hiyo kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Jambo hilo ndilo lililomfanya Onana aondolewe kwenye nafasi ya kuwa kipa namba moja wa Man United na kocha Amorim, 40, kuanza kumtumia Altay Bayindir, akimwanzisha kwenye mechi zote tatu ilizocheza timu hiyo kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Nafasi ya kipa huyo Mcamerooni kupata matumaini ya kucheza msimu huu yamezidi kufifia baada ya kocha Amorim kuleta kipa mwingine, alipomsajili Sene Lammens kutoka Royal Antwerp kwa ada ya Pauni 18.5 milioni katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Onana alimtibua kocha huyo Mreno baada ya kutaka mkataba wake uboreshwe baada ya wachezaji wote wa Man United kukatwa asilimia 25 ya mishahara yao kutokana na timu hiyo kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, kipengele ambacho kimechomekwa kwenye kila mkataba wa mchezaji wa miamba hiyo ya Old Trafford.
Sasa mpango wa Man United ni kumtoa kwa mkopo Onana akiwindwa na klabu ya Trabzonspor ya huko Uturuki na endapo dili hilo likifanikiwa basi atakwenda kupandisha mshahara wake huko Uturuki.
Kocha Amorim alitaka kumwamini Bayindir, lakini baada ya kufanya makosa kadhaa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, ameamua kwenda kuleta kipa mwingine, ambaye atakuwa namba moja kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.