Kumbe Dogo Janja aliyeivuruga Brazil ni mwanafunzi
Muktasari:
- Jina lake ni Ayyoub Bouaddi, kiungo huyo wa Morocco alifanya balaa katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil, akiwafanya wengi kujiuliza ni nani hasa kijana huyo ambaye alionekana kucheza bila hofu mbele ya nyota wakubwa kama Vinicius Junior, Casemiro na Bruno Guimaraes.
WAKATI mashabiki wengi wa soka duniani walitarajia kuona mastaa wa Brazil wakitawala mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco, kijana mwenye umri wa miaka 18 alivuruga hilo.
Jina lake ni Ayyoub Bouaddi, kiungo huyo wa Morocco alifanya balaa katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil, akiwafanya wengi kujiuliza ni nani hasa kijana huyo ambaye alionekana kucheza bila hofu mbele ya nyota wakubwa kama Vinicius Junior, Casemiro na Bruno Guimaraes.
Bouaddi hakuonyesha dalili za kuwa anacheza mechi yake ya kwanza ya ushindani katika timu ya taifa ya wakubwa. Badala yake, alionekana kama mchezaji mwenye uzoefu wa miaka mingi katika michuano mikubwa.
Aligusa mpira mara 88, akashinda mipira ya kugombania mara 11 na kukamilisha pasi 30 katika nusu ya uwanja wa Brazil huku akimaliza mchezo akiwa na usahihi wa pasi wa asilimia 93.
Kwa wengi, alikuwa mchezaji bora mchezo licha ya Vinicius Junior kupewa tuzo rasmi ya mchezaji bora wa mechi.
KUTOKA UFARANSA HADI MOROCCO
Bouaddi alizaliwa Juni 2, 2007 katika mji wa Creil nchini Ufaransa akiwa na asili ya Morocco.
Baba yake Hassan Bouaddi aliwahi kuwa Naibu Meya wa mji huo, huku mtoto wake akianza kucheza soka katika klabu ya AFC Creil kabla ya kujiunga na akademi ya Lille akiwa na umri wa miaka 13.
Akiwa mdogo, makocha wake walivutiwa na namna alivyokuwa akicheza kwa utulivu kuliko umri wake. Uwezo wake wa kupokea mpira, kupiga pasi na kusoma mchezo ulimtofautisha na vijana wengine.
Ndani ya muda mfupi, aligeuka kuwa moja ya vipaji vinavyopewa thamani kubwa zaidi nchini Ufaransa.
ALIANDIKA HISTORIA AKIWA NA MIAKA 16
Machi 2023, siku tatu tu baada ya kutimiza miaka 16, Bouaddi alipata nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha Lille.
Hatua hiyo ilimfanya kuwa mmoja wa wachezaji wachanga zaidi kuwahi kuichezea klabu hiyo katika historia yake.
Baadaye aliweka rekodi nyingine kwa kuwa mmoja wa wachezaji wenye umri mdogo zaidi kushiriki michuano ya Ulaya. Kuanzia hapo, maendeleo yake yalikuwa makubwa.
SIKU ALIYOIFUNGA REAL MADRID
Moja ya mechi zilizobadilisha maisha yake ilikuwa Oktoba 2024. Siku hiyo Bouaddi alikuwa ametimiza miaka 17 na Lille ilikuwa ikicheza dhidi ya Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Badala ya kuogopa majina makubwa yaliyokuwa mbele yake, alicheza kwa kujiamini na kusaidia Lille kupata ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya mabingwa hao wa Hispania.
Baada ya mechi, mashabiki wa Lille walimzunguka na kumuimbia wimbo wa kumtakia heri ya kuzaliwa.
Tangu siku hiyo, jina lake lilianza kuzungumzwa katika klabu kubwa za Ulaya.
ALIIKATAA UFARANSA
Kama ilivyokuwa kwa nyota wengi wenye asili ya Afrika waliozaliwa Ulaya, Bouaddi alikuwa na nafasi ya kuichezea Ufaransa.
Lakini Morocco ilifanya kazi kubwa kuhakikisha haimpotezi.
Kocha Mohamed Ouahbi amefichua kuwa walifanya mikutano mingi na mchezaji huyo kabla ya Kombe la Dunia ili kumshawishi kuichagua Morocco.
Hatimaye alikubali na sasa anaonekana kuwa moja ya silaha muhimu za taifa hilo katika miaka ijayo.
Uamuzi huo unaonekana kuwa ushindi mkubwa kwa Morocco, hasa baada ya kiwango alichokionyesha dhidi ya Brazil.
DARASANI PIA NI NYOTA
Kinachomfanya Bouaddi kuwa tofauti zaidi na wachezaji wengi wa umri wake ni kwamba bado anaendelea na masomo.
Licha ya kucheza soka la kulipwa katika kiwango cha juu kabisa barani Ulaya, Bouaddi anaendelea kusomea shahada ya Hisabati na Fizikia.
Mchezaji huyo amewahi kueleza kuwa elimu ni sehemu muhimu ya maisha yake na humsaidia kufikiria vizuri zaidi ndani na nje ya uwanja.
"Nataka kutumia muda wangu vizuri. Masomo yananisaidia kuifanya akili yangu kuwa makini zaidi," amewahi kusema.
Kabla hajawa nyota wa soka, aliwahi kushinda shindano la hotuba kwa wanafunzi wa akademi za soka nchini Ufaransa, jambo lililoonyesha mapema kuwa alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili.
VIGOGO WAMTOLEA MACHO
Baada ya kung'ara dhidi ya Brazil, vigogo wa soka Ulaya wameendelea kumfuatilia kwa karibu.
Arsenal inatajwa kuonyesha nia ya kumsajili huku Paris Saint-Germain, Bayern Munich na Liverpool nazo zikihusishwa na dili hilo.
Lille inaaminika kumthaminisha kwa zaidi ya Pauni 70 milioni kutokana na uwezo wake na umri wake mdogo.
Kwa miaka 18 tu, Bouaddi tayari ameonyesha uwezo wa kucheza dhidi ya viungo bora duniani bila kuogopa.