Mashabiki Japan watoa somo kubwa nje ya uwanja, Simba,Yanga kunalakujifunza
Muktasari:
- Mashabiki wa Japan wameendelea kuonyesha kwa nini wanatajwa kuwa miongoni mwa mashabiki wenye nidhamu zaidi duniani baada ya kitendo cha kusafisha taka katika Uwanja wa AT&T jijini Dallas, Marekani, kufuatia mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi.
VUTA picha siku moja mashabiki wa Simba na Yanga wakimaliza Dabi ya Kariakoo kisha wakabaki uwanjani kuokota chupa, makaratasi na taka nyingine kabla ya kuondoka. Inaweza kuonekana kama hadithi ya kufikirika lakini ndivyo ilivyotokea kwa mashabiki wa Japan katika Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani.
Mashabiki wa Japan wameendelea kuonyesha kwa nini wanatajwa kuwa miongoni mwa mashabiki wenye nidhamu zaidi duniani baada ya kitendo cha kusafisha taka katika Uwanja wa AT&T jijini Dallas, Marekani, kufuatia mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi.
Maelfu ya mashabiki wa Japan waliokuwa wamevalia rangi za timu yao walishuhudia mchezo huo wa Kundi F ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2 lakini baada ya filimbi ya mwisho hawakukimbilia maegesho ya magari au mabasi ya kurejea makwao.
Badala yake, walitoa mifuko ya taka waliyoibeba na kuanza kusafisha sehemu walizokuwa wamekaa.
Katika mchezo huo, nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk, aliitanguliza mbele timu yake kabla ya Keito Nakamura kuisawazishia Japan.
Crysencio Summerville aliirejeshea Uholanzi uongozi, lakini Koki Ogawa aliipa Japan bao la kusawazisha lililowahakikishia pointi moja muhimu.
Hata hivyo, matokeo ya mchezo huo yalifunikwa na picha za mashabiki wa Japan wakikusanya vikombe vya kahawa, mifuko ya vitafunwa, makaratasi na taka nyingine zilizokuwa zimeachwa kwenye viti vya watazamaji.
Kilichowashangaza wengi ni kwamba mashabiki hao walifika uwanjani tayari wakiwa na mifuko maalumu ya taka, jambo linaloonyesha kuwa kufanya usafi baada ya mechi si jambo la bahati mbaya, bali ni sehemu ya utamaduni wao.
Katika fainali za Kombe la Dunia la Qatar 2022 mashabiki hao walijizolea sifa baada ya kusafisha sehemu zao za kukalia hata baada ya ushindi dhidi ya Ujerumani.
Vilevile, katika Kombe la Dunia la 2018 nchini Russia walifanya jambo hilo baada ya ushindi dhidi ya Colombia huku tabia hiyo baadaye ikianza kuigwa na mashabiki wa mataifa mengine, ikiwemo Senegal.
Si mashabiki pekee wanaobeba sifa hizo. Wachezaji wa Japan pia wamewahi kusifiwa kwa kuacha vyumba vya kubadilishia nguo vikiwa safi kabisa baada ya mechi, wakati mwingine wakiacha hata ujumbe wa shukrani kwa wenyeji wa mashindano.
Kwa mujibu wa wataalamu wa jamii nchini Japan, usafi ni sehemu ya maisha ya kila siku. Watoto hufundishwa tangu shule za msingi kuwajibika kusafisha madarasa yao, korido na mazingira ya shule, jambo ambalo hujenga tabia ya kuthamini usafi hata wanapokuwa watu wazima.
Ndiyo maana kila Japan inaposhiriki mashindano makubwa ya kimataifa, mashabiki wake huendelea kuonyesha kuwa soka siyo tu kuhusu mabao, ushindi au vikombe, bali pia ni nafasi ya kuonyesha maadili, nidhamu na heshima kwa jamii inayokuzunguka.
Na pengine swali la kujiuliza ni hili, je, siku moja mashabiki wa Tanzania wataiga mfano huo na kuacha viwanja vyetu vikiwa safi baada ya mechi kubwa? Kama Japan wameweza, kwa nini isiwezekane kwetu pia?