Kuhusu Man United... Thierry Henry kasema wewe nani ubishe!

MANCHESTER, ENGLAND. GWIJI wa Arsenal, Thierry Henry amesema anaamini jiniazi Erik ten Hag ataifanya Manchester United kucheza soka la kuvutia kuliko hata walipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson na kwamba ndani ya mwaka mmoja tu, miamba hiyo ya Old Trafford itakuwa tishio kubwa uwanjani.

Supastaa huyo wa Ufaransa, Henry alivutiwa na namna Man United walivyoweza kuichezea mechi ya Arsenal licha ya kufungwa 3-2 uwanjani Emirates, Jumapili iliyopita. Henry alisema anamkubali sana Ten Hag na maujuzi yake ndani ya uwanja na aliwahi kumpendeza huko Barcelona wamchukue wakati walipoachana na Ronald Koeman - kwamba alifaa kuliko Xavi, aliyeteliwa Novemba 2021.

Henry alikiri kushangazwa na namna Man United ilivyoweza kukabiliana na presha ya Arsenal na alisema hivi: “Nimefurahi Arsenal kushinda na walistahili kutokana na kiwango chake kile hasa katika kipindi cha pili. Lakini, hawa Man United wamekuwa tofauti sana chini ya Ten Hag.

“Nitakuwa mkweli, mimi ni shabiki mkubwa wa Ten Hag na nampenda sana. Ni kocha niliyemshauri rais wa Barcelona, Joan Laporta amchukue wakati walipomfukuza Koeman. Yule jamaa ni jiniazi.

“Tuliona timu iliyoandaliwa kwa miaka mitatu dhidi ya timu iliyoandaliwa kwa miezi sita, pia timu iliyokuwa na wiki moja ya mapumziko dhidi ya timu iliyopumzika kwa siku mbili tu, lakini bado Man United waliweza kwenda jino kwa jino, hilo limenishangaza sana.

“Nilidhani Arsenal wakawabana sana Man United kuanzia mwanzo hadi mwisho na kwamba wachezaji wa Man United wangekaa tu nyuma, lakini nilikosea, Man United badala yake walikuwa na umiliki mzuri wa mpira hada kwenye kipindi cha kwanza.

“Mpeni mwaka mmoja tu Ten Hag na apewe sapoti sokoni kwenye usajili, Man United watakuwa balaa uwanjani. Simkosei heshima Sir Alex lakini kama Ten Hag atapewa wakati wa kufanya mambo yake kwa nafasi, Man United itacheza soka la mvuto uwanjani kuliko ilivyokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.”

Man United itarejea uwanjani leo Jumatano kukipiga na Nottingham Forest huko City Ground katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi.

Nottingham Forest na Man United kwa msimu huu zimeshakutana mara moja kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Old Trafford, ambapo wenyewe walishinda 3-0. Lakini, hii ni michuano tofauti na ipo kwenye hatua ya nusu fainali, licha ya kuchezwa kwa staili ya nyumbani na ugenini.

Mechi ya marudiano itapigwa Februari Mosi huko Old Trafford, wakati Januari 28, Man United itakipiga na Reading kwenye Raundi ya Nne ya Kombe la FA.

Mechi zijazo Man united
-Januari 25 vs Nottm Forest (ugenini)
-Januari 28 vs Reading (nyumbani)
-Februari 1 vs Nottm Forest (nyumbani)
-Februari 4 vs Crystal Palace (nyumbani)
-Februari 8 vs Leeds United (nyumbani)
-Februari 12 vs Leeds United (ugenini)