KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Umri na majeraha vinavyo husiana!

New Content Item (2)
New Content Item (2)

HEKAHEKA za mchezaji yupi ataitwa kwenye timu za taifa ambazo zimefuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika nchini Qatar zinazidi kupamba moto kutokana na kuibuka kwa nyota wapya na huku pia kukiwa na mastaa wa zamani.

Wapo nyota wa zamani ambao umri umewatupa mkono wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 30 lakini bado viwango vyao bado vinawafanya baadhi ya makocha wa timu za taifa kuwa na kigugumizi cha kuwaacha.

Mastaa ambao umri wa kisoka ambao unaonekana kuwatupa mkono ikiwamo Cristiano Ronaldo wa timu ya taifa ya Ureno, Lionel Messi Argentina, Zlatan Ibrahimovic Sweden, Gianluigi Buffon Italia, James Milner England, Thiago Silva Brazil na Diego Godin Uruguay,

Wengine ni pamoja ni Luca Modric Croatia, Sergio Ramos Hispania, Pepe Ureno, Olivier Giroud Ufaransa, Giorgio Chielini Italia na Guillermo Ochoa (Mexico).

Wote hawa ni wanasoka ambao wana umri wa zaidi ya miaka 30 na huenda hizi zikawa ndio mashindano yao ya mwisho ya Kombe la Dunia endapo kama wataitwa katika timu zao za taifa.

Kwa mujibu wa tafiti zilizowahi kufanywa katika soka zinaonyesha umri wa juu wa mwanasoka kucheza kwa kiwango ni wastani wa umri wa miaka 28-29.

Tafiti maarufu ni ile iliyowahi kutolewa na mtandao wa frontiersin mwaka 2019 ambao ulifanywa katika ligi nne bora za Ulaya ikiwamo Bundesliga, EPL, la Liga na Serie A.

Tafiti hiyo ilionyesha kuwa wachezaji wengi walikuwa katika kiwango cha juu katika umri wa miaka 21-29. Na baada ya umri wa miaka 29 kuendelea viwango vyao nilianza kuporomoka.

Wachezaji walio wengi wa soka wanaonyesha wanapofikisha umri wa miaka 29- 30 kuendelea utimamu wa kimwili unapungua ikiwamo kupungua kwa kasi, nguvu na ustahimilivu wa misuli.

Kwa upande wa jicho la kitabibu wachezaji wenye umri mkubwa miili yao inakosa ustahimilivu dhidi ya majeraha yatokanayo na michezo ikiwamo majeraha ya misuli yanayotokana na kutumika sana.

Kuitwa au kutokuitwa katika timu za Taifa zinazoshiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 kutategemea na mipango ya kocha na benchi lake la ufundi.

Ingawa suala la umri lazima benchi la ufundi litazingatiwa katika mipango yao ikiwamo nani aachwe na nani abebwe.

Hii ni kutokana na kufahamu kuwa utimamu wa mwili hupungua na huku pia wakipata majeraha kirahisi kutokana na kutumika sana katika klabu zao pamoja na timu zao za taifa.

Uzoefu wa kisaikolojia unaonyesha wachezaji wa kulipwa wa umri wa zaidi ya miaka 30 ambao wamepata mafanikio makubwa ari ya kujituma inapungua kutokana na kubweteka na mafanikio waliyopata.

Umri na soka iko hivi

Msemo wa Afya ni mtaji hata katika soka unazingatiwa kwani afya ya mchezaji ndio kila kitu kwa mchezaji kuitwa timu ya taifa kwani kadiri umri unavyokuwa mkubwa ndivyo pia hatari ya kupata majeraha kwa mchezaji inakuwa kubwa.

Ni kawaida kwa wachezaji wa soka duniani wanapofikisha umri miaka 30 kuanza kuitwa wazee hii ni kutokana na sababu za kitaalam kuwa mwili nao unakuwa umegota ukuaji.

Nafasi wanazocheza wanasoka na umri wao ni moja ya kitu muhimu. Tafiti zinaonyesha washambuliaji na viungo ndio wanaporomoka mapema wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 29 ukilinganisha makipa na mabeki.

Hata makocha wa timu za taifa hupendelea kuwa na wingi wa wachezaji vijana na huku wakiwachukua wachezaji wachache wenye umri mkubwa ili kuleta uzoefu na hamasa katika timu.

Mfano mshambuliaji wa soka wa klabu ya PSG, Lionel Messi umri si kitu kwani pamoja na kuwa na umri wa miaka 34 lakini bado ni nguzo katika timu ya taifa ya Argentina.

Ukija kwa Cristiano Ronaldo, 37, ambaye siku za karibuni kiwango chake katika klabu ya soka ya Manchester United kimekua kikisuasua lakini bado ni vigumu kwa kocha wa Ureno kumuweka pembeni.

Mastaa kama hawa umri umewatupa lakini uwepo wao timu ya taifa ni tiba ya kisaikolojia kwa wachezaji wa timu ya taifa kwani uwepo wao unaleta hamasa na huku wakiwapa hofu timu pinzani.

Kipengele cha umri wa mastaa wengi kinaonekana kufumbiwa macho hii ni kutokana na mafanikio aliyoyapata na bado anaonekana kuwa umri huo si lolote kwani anaonekana bado uwezo wao ni mkubwa.

Katika miaka hiyo wanapoitumikia klabu na timu za taifa misuli ya mwili na viungo vingine vinakuwa vimetumika sana na huku pia kukitokea majeraha ya hapa na pale.

Lakini uimara na kudumu kwa mchezaji akiwa na kiwango kile kile hutofautiana mchezaji na mchezaji ikiwamo asili ya mwili, aina ya mazoezi au mfumo wa mafunzo, majeraha anayopata, lishe, kuugua magonjwa mengine na miendendo na mitindo ya kimaisha anayoishi.

Vile vile kudumu huko kunaweza kuchangiwa na ligi anayocheza, mazingira ya kijiografia ya nchi au ligi anayocheza na huduma za uponyaji anazopata pale anapokuwa mgonjwa au majeruhi.

Iko hivi kucheza soka na umri zaidi ya miaka 30

Kwa kawaida viungo vya mwili wa binadamu ikiwamo maungio, misuli, mifupa, mishipa ya fahamu na damu hupungua uimara kadiri umri unavyosonga.

Kitabibu viungo vya mwili kama vile mfupa ukuaji wake kwa wanadamu wengi huishia pale mtu anapofika umri wa miaka 25. Umri ukishapiga hatua hata mfumo wa usagaji chakula nao unakuwa dhaifu kiutendaji.

Pia ipo tofauti kubwa kwa mchezaji aliye majeruhi mwenye umri wa chini ya miaka 30 na yule mwenye zaidi ya miaka 30, hapa anayepona majeraha mapema ni mwenye umri mdogo.

Moja ya vitu ambavyo vinachangia kutopona majeraha kwa wakati ni umri wa mchezaji majeruhi hii ni kutokana viungo hivyo vinakuwa vimetuma sana na kuchakaa.

Pamoja ya kwamba tishu za mwili wa binadamu hufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa sana lakini pale zinapofanyishwa kazi kupita kiasi huweza kuwa chanzo cha wanasoka wa aina hii kupata Majeraha.

Kadiri mwili unavyotumikishwa ndivyo pia unakuwa katika hatari zaidi ya kupata majeraha mbalimbali ikiwamo ya misuli, mifupa na nyuzi ngumu yaani ligamenti na tendoni.

Ili mchezaji kuweza kumudu jambo hili umri alionao una maana kubwa, wanasoka wanapofikisha umri zaidi ya miaka 30 tayari mwili unakosa uimara ukilinganisha wanapokuwa na umri wa miaka 17-30.

Wachezaji wanapotumika sana miili yao huweza kuambatana na majeraha wakati wanashiriki mazoezi na mashindano mbalimbali.

Tusubiri nini kitajiri kufikia tarehe 20 Novemba 2022 siku ya ufunguzi tuone ni wachezaji gani wenye umri wa zaidi ya miaka 30 watakuwepo Qatar.