KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Mziki upo ndani humu

DOHA, QATAR. YULE mwali anayesakwa huko Qatar vita yake itapigwa humu. Ni mchakamchaka.

Viwanja nane vitawaka moto huko Qatar katika fainali za kwanza za Kombe la Dunia zitakazopigwa Mashariki ya Kati. Viwanja hivyo, saba ni vipya kabisa zimejengwa kuzunguka mji wa Doha. Mechi 64 zitapigwa kumsaka mwali huyo wa Qatar.

Fainali zenyewe za Kombe la Dunia 2022 zitaanza Novemba 20 hadi Desemba 18. Ni fainali za 22 tangu kuanzishwa kwake ambapo atasakwa bingwa wa dunia. Mara ya mwisho, Kombe la Dunia kufanyika Asia ilikuwa 2002 Japan na Korea Kusini.

Lakini, huko Qatar mzigo utapigwa kwenye viwanja vinane vilivyopo kwenye miji mitano, ambapo mataifa 32 yatachuana kwenye mechi 64 kumpata bingwa mmoja.

Viwanja mahususi kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar ni Lusail Iconic uliopo Lusail, Al Bayt Stadium uliopo Al Khor, Al Janoub Stadium uliopo Al Wakrah, Ahmad Bin Ali Stadium, Khalifa International Stadium na Education City Stadium vilivyopo kwenye mji wa Al Rayyan na Stadium 974 na Al Thumama Stadium vinavyopatikana Doha.

Viwanja vyote hivyo vimejengwa ndani ya eneo la kilomita 55 kuzunguka mji mkuu wa Qatar, Doha.

Uwanja wa Khalifa International umekuwa ukitumika tangu 1976, lakini viwanja vingine vyote vilijengwa ndani ya miaka mitatu kwa ajili ya fainali hizo za Kombe la Dunia. Khalifa utatumika kwenye mechi za kutafuta mshindi wa tatu miongoni mwa mechi zitakazocheza.

Lusail Iconic ndiyo wenye uwezo wa kuingiza watu wengi zaidi, watazamaji 80,000. Na ndiyo uwanja utakaokuwa bize zaidi kwenye fainali hizo kutokana na kwamba zitachezwa mechi 10, ikiwamo fainali na sherehe za kufunga mashindano.

Al Bayt Stadium, utatumika kwenye mechi tisa, utatumika pia kwenye sherehe za ufunguzi wa fainali hizo za Kombe la Dunia 2022, ambapo mechi ya kwanza itawashuhudia wenyeji Qatar watakaokipiga na Ecuador, Novemba 20.

Mechi za makundi zimegawanywa kwenye viwanja kama ifuatavyo:

Kundi A, B, E na F: Al Bayt Stadium, Khalifa International Stadium, Al Thumama Stadium, Ahmad bin Ali Stadium

Kundi C, D, G na H: Lusail Iconic Stadium, Stadium 974, Education City Stadium, Al Janoub Stadium

Viwanja hivyo vya Qatar vina teknolojia bora kabisa ya kufanya hali ya hewa kuwa ya kawaida kwa mashabiki na wachezaji watakaokuwa uwanjani.