KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Makocha hawa wasipotoboa, watafukuzwa mapema

DOHA, QATAR. KUELEKEA fainali za Kombe la Dunia Qatar, Novemba mwaka tutashuhudia matukio mengi na kihistoria ndani na nje ya uwanja. Kubwa linalosubiriwa hasa ni kocha yupi ambaye atatoboa na kusonga mbele kwenye fainali hizo.

Aidha wapo makocha wenye presha kubwa kutokana na mwenendo mbovu wa timu kabla ya fainali hizo, mfano Gareth Southgate na kikosi chake cha England. Kwa sasa Southgate amekalia kuti kavu na endapo atashindwa kuipa mafanikio England kwenye Kombe la Dunia basi atafungashiwa virago.

Hawa hapa makocha waliokalia kuti kavu na endapo watashindwa kutoboa Kombe la Dunia.


GARETH SOUTHGATE - ENGLAND

Licha ya kufanya vizuri Euro na kutinga fainali mwaka jana, kocha huyu amekalia kuti kavu baada ya kuonyesha kiwango kibovu kwenye Michuano ya Nations League, England ikishuka daraja la pili (League B) ya michuano hiyo ya mataifa Ulaya inayohusisha League A, B, C, na D. Hii ni rekodi mbovu zaidi kwa England katika miaka 30 iliyopita ikicheza michezo mitano ya Group 3 la League A ya michuano hiyo bila kupata ushindi. Msimu ujao England itashiriki Daraja la Pili. Aidha kwa upande wa Southgate anaelewa kabisa endapo atashindwa kupata mafanikio Qatar basi kibarua chake kitaota nyasi.


LOUIS VAN GAAL - UHOLANZI

Tofauti na Southgate kocha huyo amefanya vizuri akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa Uholanzi hususan kwenye Michuano ya Nations League mwaka huu.Mpaka sasa Uholanzi haijapoteza mchezo katika hatua ya makundi ya michuano hiyo. Uholanzi inaongoza Kundi 4 ikiwa na pointi 16 ikifuatiwa na Ubelgiji yenye pointi 10 baada y ushindi wa bao 1-0 ilioupata dhidi ya Ubelgiji. Aidha Van Gaal ana kazi kubwa ya kuhakikisha Uholanzi inafanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu kwani mashabiki wanatarajia mambo makubwa kutoka kwake baada ya kuonyesha dalili nzuri kwenye Michuano ya Nations League.


HANS FLICK - UJERUMANI

Flick ni miongoni mwa makocha ambao wamekikalia kuti kavu hasa kutokana na mwenendo mbovu wa Ujerumani kwenye Michuano ya Nations League lakini miamba hiyo haikufanya vizuri na inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi 3 baada ya kujikusanyika pointi 6.

Ujerumani imeweka rekodi mbovu kwenye michuano hiyo ya mwaka huu.Katika michezo mitano Ujerumani imepata ushindi mara mbili tu, sare moja na kufungwa mara moja. Mashabiki wa Ujerumani wameonyesha hofu kuelekea fainali za Kombe la Dunia jambo ambalo limempa presha kocha huyo.


DIDIER DESCHAMPS- UFARANSA

Unaweza kujiuliza kwa nini Deschamps yupo kwenye orodha hii ukweli ni kwamba kocha huyu kibarua chake kipo mkononi mwake kuelekea fainali za Kombe la Dunia.

Tayari ameonyesha taswira mbovu kwenye Michuano ya Nations League hatua ya makundi, ikumbukwe Ufaransa ndio mabingwa watetezi wa Nations League na Kombe la Dunia. Hivi karibuni Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliweka wazi anatamani kumuona Zinadine Zidane akiwa kocha mkuu wa Ufaransa.

Kauli hiyo si nzuri kwa upande wa Deschamps na hatima yake itategemea na mafanikio atakayoipa Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Qatar.


LUIS ENRIQUE- HISPANIA

Ndoto ya Enrique ni kuipa Hispania ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kuikacha Manchester United ilipoonyesha nia ya kuhitaji huduma yake kabla ya haijampata Erik ten Hag. Ndoto ya Enrique huenda ikazimika endapo atashindwa kuifikisha Hispania mbali kwenye fainali hizo zitakazofanyika Qatar. Hispania ina kabarua kigumu dhidi ya Ureno leo Jumanne kwenye mechi ya mwisho hatua makundi ya Nations League.