Kombe la Dunia lipo ofisini kwa Rais Trump
Muktasari:
- Rais Trump alikuwapo uwanjani MetLife, New Jersey, Jumapili iliyopita kwenye mchezo wa fainali wakati Chelsea ilipoichapa Paris Saint-Germain mabao 3-0.
NEW YORK, MAREKANI: RAIS wa Marekani, Donald Trump amefichua kwamba ofisi zake za Oval ndiko lilipo taji la Kombe la Dunia la Klabu limehifadhiwa.
Rais Trump alikuwapo uwanjani MetLife, New Jersey, Jumapili iliyopita kwenye mchezo wa fainali wakati Chelsea ilipoichapa Paris Saint-Germain mabao 3-0.
Na alijumuika kwenye jukwaa wakati The Blues ilipokuwa ikisherehekea kushinda taji hilo la ubingwa wa dunia. Lakini, tangu fainali hiyo ilipopigwa, taji hilo lipo Ikulu.
Trump, 79 alisema kwamba amekuwa akilitunza taji hilo baada ya rais wa Fifa, Gianni Infantino kumwambia watatengeneza kombe jingine la pili.
Akizungumza na Dazn, Rais Trump alisema: “Niliwaambia, lini mnakuja kuchukua hili kombe? ‘Waliniambia hawatakuja kulichukua. Unaweza kuwa nalo ofisini Oval. Tutatengeneza jingine.’ Na walitengeneza jingine kwa ajili ya Chelsea. Hiyo ilivutia sana, lakini kwa sasa taji orijino lipo Oval.”
Kama mataji hayo mawili yanafanana hilo bado halifahamiki. Infantino alitambulisha taji hilo, ambalo lilikuwa na kimo cha inchi 17 na uzito wa karibu kilo tano, Machi mwaka huu kwenye ofisi ya Oval. Fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026, zitafanyika pia Marekani pamoja na ushiriki wa nchi nyingine za Mexico na Canada.