KOMBE LA DUNIA 2022: Ubelgiji kwa uwezo tu, subirini muone

DOHA, QATAR. UBELGIJI ilianza kuonja mafanikio ya Kombe la Dunia 1982 ilipowachapa mabingwa watetezi Argentina kwa bao 1-0 na kuongoza kundi. Hata hivyo, fainali zilizofuata ilikuwa ngumu kutoboa kwani ilipoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Poland na Sovient Union.

Katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika 1986 Ubelgiji haikuwa vizuri na ilimaliza katika nafasi ya tatu katika kundi.

Lakini licha ya kutofanikiwa kwa asilimia kubwa imewahi kuweka historia ya kufuzu michuano mara tatu, ila haikufanikiwa kusonga mbele. Mwaka 2002 ilikaribia kufuzu, lakini ikaangukia mikononi mwa Brazil. Ubelgiji imeendelea kuimarika kadri miaka inavyozidi kwenda. Kocha anayeinoa kwa sasa Roberto Martinez anakifua kikosi chake na kilifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika fainali zilizofanyika Russia baada ya kuichapa England.


KWANINI UBELGIJI?

Ubelgiji ina mastaa wanaotegemewa katika kikosi cha kwanza cha Martinez ambaye mara nyingi amekuwa akiwatumia katika mashindano mbalimbali.

Kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois ni bora ndani ya kikosi cha Ubelgiji kwa sasa na ana kazi kubwa ya kulibeba taifa lake katika fainali za Kombe la Dunia Qatar, kwani akiwa na umri wa miaka 30 tayari amecheza mechi 96 na ni mchezaji muhimu kikosini kwa sababu aliwahi kubeba tuzo ya kipa bora. Staa mwingine ni Kevin De Bruyne, kiungo ambaye ni nahodha wa taifa hilo baada ya Eden Hazard kuvuliwa kitambaa hicho.

De Bruyne ni injini ya timu anayetegemewa katika eneo la kiungo mshambuliaji na mkali wa asisti. Nyota huyo ameifungia mabao 25 Ubelgiji katika mechi 100 alizoichezea katika mashindano.

Mchezaji huyo anashika rekodi ya ufungaji bora wa muda wote Ubelgiji akiwa na uwezo wa kufunga mabao anapokuwa popote. Naye Romelu Lukaku aliyeng’ara katika fainali za Kombe la Dunia 2018, alilifungia mabao manne akilisaidia taifa lake kushika nafasi ya tatu mwaka huo. Lukaku ni aina ya wachezaji wenye uwezo wa kufunga kila aina ya mabao, hivyo Ubelgiji itafaidika na ubora wake katika fainali hizo.Mastaa hao wanategemewa kufanya makubwa katika kikosi hicho.