Kodi zampukutisha Anthony Joshua
Muktasari:
- Bondia huyo kutoka England alipigana Paul usiku wa kuamkia Jumatatu katika ukumbi wa Kaseya Center huko Miami, Florida, Marekani pambano lililorushwa mubashara kupitia Netflix.
FLORIDA, MAREKANI: LICHA ya kumchapa Jake Paul kwa KO, bondia Anthony Joshua ameripotiwa kuwa atapoteza pesa nyingi ambazo ni karibu ya nusu ya malipo yake ya Pauni 70 milioni aliyopata katika pambano hilo.
Bondia huyo kutoka England alipigana Paul usiku wa kuamkia Jumatatu katika ukumbi wa Kaseya Center huko Miami, Florida, Marekani pambano lililorushwa mubashara kupitia Netflix.
Pambano hilo lilipangwa kudumu kwa raundi nane, lakini Joshua alishinda katika raundi ya sita kwa kumtandika Paul, ambaye alivunjika taya mara mbili na hakuweza kusimama baada ya kuhesabiwa na mwamuzi.
Joshua sasa amefikisha rekodi ya kushinda mapambano 29 kati ya 33 aliyopigana ikiwa ni ushindi wa kwanza tangu alipochapwa na Daniel Dubois kwenye Uwanja wa Wembley Septemba mwaka jana.
Baada ya ushindi huo, Joshua ameripotiwa kutaka kupigana na Tyson Fury mwakani.
Fury alitangaza kustaafu ndondi Januari mwaka huu, baada ya kupoteza mapambano mawili mfululizo dhidi ya Oleksandr Usyk.
Kwa upande wa Paul ambaye alifanyiwa upasuaji baada ya pambano hilo la Miami, alikuwa akipoteza kwa mara ya pili tangu aanze kucheza ndondi mwaka 2020.
Sasa, katika pambano hilo, pesa iliyowekwa mezani kwa ajili ya malipo ya mabondia hao wawili inatajwa kuwa ni Pauni 137 milioni, na kwa mgawanyo Joshua alitakiwa kupata takribani Pauni 70 milioni.
Hata hivyo, Joshua akapata nusu ya pesa hiyo kutokana na kodi kubwa ambayo itakatwa kutoka kwenye pesa hiyo.
Kulingana na taarifa za vyombo mbalimbali vya habari ni kwamba, Joshua atalazimika kutozwa kodi Marekani na Uingereza, ikimaanisha takriban Pauni 33 milioni zitamezwa na kodi ya serikali ya Marekani, malipo kwa HMRC na michango ya Bima ya Taifa (National Insurance) England.
Taarifa hiyo imesema: "Utafiti kutoka kwa wataalamu wa data wa AceOdds umebaini kwamba katika Pauni 70 milioni ambazo Joshua amezipata atakatwa kodi jumla ya Pauni 31 milioni."
"Mgawanyo wa gharama hiyo utagawanywa kati ya mamlaka za kodi za Marekani na Uingereza, ambapo ni asilimia 37 ya mapato yake ambapo Pauni 25,867,333 itapelekwa moja kwa moja kwa IRS kufidia kodi ya Marekani ya Joshua."
"Ingawa Florida haina kodi ya jimbo, serikali ya Marekani inatoza kodi ya mapato kwa kiwango cha juu cha asilmia 37. Kwa kuwa pambano lilifanyika kwenye ardhi ya Marekani, Joshua atalazimika kulipa kodi hiyo. Joshua pia atalazimika kulipa kodi ya nchini England ambayo inakadiriwa kuwa ni Pauni 5,618,870.
“Kutokana na mapato yake yote, Joshua pia atalazimika kulipa Pauni 1,401,257 kwa ajili ya kuchangia bima ya afya ya taifa. Baada ya kulipa vyote hivyo, Joshua atabaki na Pauni 37,112,540, sawa na asilimia 53 tu ya Pauni 70 milioni alizovuna."