Kocha Zambia aiwahi AFCON baada ya kula msosi wenye sumu
Muktasari:
- Zambia itavaana na Mali, mjini Casablanca katika pambano la Kundi A la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, baada ya wenyeji Morocco kuanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Comoros jana Jumapili huko Rabat.
KOCHA wa Zambia, Moses Sichone, leo Jumatatu atapata fursa ya kukaa benchi na kuiongoza timu yake kwa mara ya kwanza, baada ya kukosa mechi yake ya kwanza mwezi uliopita.
Zambia itavaana na Mali, mjini Casablanca katika pambano la Kundi A la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, baada ya wenyeji Morocco kuanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Comoros jana Jumapili huko Rabat.
Sichone aliteuliwa Novemba kuchukua nafasi ya Avram Grant, aliyeacha ngazi kuinoa Chipolopolo Zambia mwishoni mwa Oktoba kufuatia mfululizo mbaya wa matokeo katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026, ikiwa ni miezi miwili kabla ya kuanza kwa AFCON 2025.
Beki huyo wa zamani wa Bundesliga aliugua ghafla baada ya kudaiwa kula sumu ya chakula (food poison) na kulazimika kulala kitandani akiwa mgonjwa wakati Zambia ilipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini.
Pia alilazwa hospitalini wakati timu yake ilisafiri kwenda Angola kwa ajili ya mechi nyingine ya maandalizi, lakini leo atakuwa benchi katika mechi ya kwanza ya AFCON 2025 dhidi ya Mali kabla ya baadae kuja kucheza na Morocco na Comoros waliopangwa kundi moja la A.
Michuano hiyo ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957 inashirikisha jumla ya timu za taifa 24 ikiwamo Tanzania inayoshiriki fainali hizo kwa mara ya nne sasa baada ya 1980, 2019 na 2023.