Kocha wa EPL afikishwa mahakamani, matatani kufilisiwa
Muktasari:
- Dowie ambaye ni mchezaji wa zamani na meneja wa soka, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu katika wiki chache zijazo baada ya kufunguliwa kesi ya kufilisika.
Aliyekuwa kocha wa timu ya Ligi Kuu ya England (EPL), Iain Dowie mwenye umri wa miaka 60, anakabiliwa na uwezekano wa kufilisika baada ya kufikishwa mahakamani na mamlaka ya kodi (HMRC).
Dowie ambaye ni mchezaji wa zamani na meneja wa soka, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama Kuu katika wiki chache zijazo baada ya kufunguliwa kesi ya kufilisika.
Dowie, anayejulikana zaidi kwa kubuni neno “bouncebackability” alipokuwa akiifundisha Crystal Palace, ambalo liliongezwa kwenye Kamusi ya Kiingereza ya Oxford mwaka 2005, anakabiliwa na hatua hiyo mpya ya kisheria takribani miongo miwili tangu alipohusishwa na mzozo wa gharama kubwa wa kisheria na klabu hiyo.
Mnamo mwaka 2007, mahakama iliamua kuwa Dowie aliidanganya Crystal Palace ili isitoze kifungu cha fidia cha pauni milioni moja alipoondoka Selhurst Park na kujiunga na Charlton Athletic.
Chanzo kimoja cha karibu, kilidokeza kuwa matatizo ya kifedha anayokabiliana nayo Dowie kwa sasa yanaweza kuwa yamechochewa na mzozo huo wa zamani.
“Inaonekana matatizo ya kifedha ya Iain yanatokana na kesi ile ya muda mrefu, hakuna sababu nyingine inayoonekana,” chanzo hicho kimeiambia The Sun.
“Ni jambo la kusikitisha kwa sababu yeye ni mtu mzuri sana. Hakuweza kunufaika na kazi za uchambuzi wa soka kama wachezaji wenzake wa zamani, lakini Iain ni mtu mwenye akili. Ikiwa kuna mtu anayeweza kujinasua, basi ni yeye.”
Katika taaluma yake ya ukocha, Dowie aliwahi kuzifundisha klabu kadhaa ikiwemo Oldham Athletic, Crystal Palace, Charlton, Coventry City na Hull City.
Kipindi chake na Crystal Palace, ndicho kinachokumbukwa zaidi, kwani aliiongoza timu hiyo kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu mwaka 2004 na kubuni msemo maarufu “bouncebackability” ambao uliongezwa kwenye Kamusi ya Kiingereza ya Oxford mwaka 2005.
Baada ya kustaafu ukufunzi, Dowie alifanya kazi kama mchambuzi wa soka wa Sky Sports na baadaye akaamua kujikita katika shughuli za kiofisi nje ya michezo.
Mwaka 2023, alifichua kuwa amejiunga na kampuni ya sheria ya Alexander Grace Law, yenye makao Lancashire, kama mkurugenzi wa biashara anayesimamia kitengo cha mikopo ya nyumba.
“Watu wanaweza kushangaa jinsi nilivyotoka uwanjani hadi ofisini, lakini nimekuwa nikifanya kazi katika sekta ya mali kwa miaka minne sasa,” alisema wakati huo.
“Nilipoombwa kujiunga, haikuwa jambo la kufikiria mara mbili.” Mkewe, Debbie, pia alihusishwa na kampuni hiyo.
Dowie alicheza zaidi ya mechi 380 na kufunga mabao 105 akiwa na klabu kama Luton Town, Southampton na West Ham, na aliwakilisha Ireland Kaskazini mara 59.
Akitambulika kwa bidii, nidhamu na akili uwanjani na nje ya uwanja, Dowie aliheshimika kwa uwezo wake wa kuijenga upya timu na kuwahamasisha wachezaji.
Mwaka 2023, alifichua kuwa alipata mshutuko wa moyo wakati wa mazoezi ya baiskeli ya spin class katika gym moja mjini Chorley, Lancashire, na akawashukuru watu waliokuwa gym na wahudumu wa dharura kwa kumwokoa.
“Niliokoka kutokana na umahiri wa kila aliyeshiriki,” alisema, na baadaye akahimiza kuongezwa kwa uelewa wa mafunzo ya CPR.
Licha ya changamoto mpya za kifedha, watu wa karibu na Dowie wanaamini bado ana nguvu ya kustahimili.