Kocha Spurs bado yupo sana mjini
Muktasari:
- Spurs imekuwa na matokeo mabaya, kiwango kipovu na kutokucheza vizuri katika mechi kadhaa za hivi karibuni na kitendo hicho kimekuwa kikiwakasirisha mashabiki na hasa baada ya kuchapwa na mahasimu wao ugenini kwenye dimba la Emirates.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya kichapo cha aibu cha mabao 4-1 kutoka kwa mahasimu wao wa London Kaskazini, Arsenal, mashabiki wa Tottenham walikuwa wanataka Kocha Thomas Frank afutwe kazi, lakini mabosi wa miamba hiyo hawana mpango huo kabisa.
Spurs imekuwa na matokeo mabaya, kiwango kipovu na kutokucheza vizuri katika mechi kadhaa za hivi karibuni na kitendo hicho kimekuwa kikiwakasirisha mashabiki na hasa baada ya kuchapwa na mahasimu wao ugenini kwenye dimba la Emirates.
Hata hivyo, inaelezwa licha ya mabosi wenyewe kukiri timu haipo vizuri bado wanataka kumpa muda zaidi kocha wakiamini anaweza kubadilisha mwenendo huo na kwa mujibu wa tovuti ya The Telegraph, familia ya Lewis ambao ni wamiliki wa klabu hiyo wanaamini Frank aliajiriwa kama sehemu ya mipango ya muda mrefu na bado msimamo huo upo, hivyo wanaona hakuna haja ya kuchanganyikiwa na kufanya maamuzi ya pupa.
Inaelezwa mabadiliko mengi ya kiufundi anayofanya Frank yamechangia mfululizo wa matokeo mabaya, huku baadhi ya wachezaji wakiwa hawakubaliani na aina ya mbinu zake.
Kikosi cha Spurs, kiliripoti kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wao wa mazoezi Jumatatu kama kawaida, kabla ya kusafiri kwenda Ufaransa kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain Jumanne.
Baada ya kufungwa na Arsenal, Frank alisema: "Mimi ni muumini mkubwa kwa mfumo wowote unaoweza kufanikiwa. Ninaelewa na niseme nitawajibika kwa matokeo yoyote yale na leo hatukucheza vizuri, hivyo mimi ndio napaswa kuulizwa. Haijalishi kama tungecheza mfumo gani, tulihitaji kuwa bora zaidi ya wapinzani wetu katika mapambano ya kuwania mpira ili kushinda mechi hii, hatukufanya hivyo lakini yote kwa yote mimi ndio mwajibikaji."
Frank alijiunga na Spurs dirisha lililopita la majira ya kiangazi kuchukua nafasi ya Ange Postecoglou aliyefungashiwa virago.
Spurs ililazimika kulipa Pauni 10 milioni kwa Brentford ili kuvunja mkataba wake na kuipata huduma yake.